
Shirika la habari la Uingereza Reuters, limeripoti kuwa ofisi ya bajeti kwenye ikulu ya rais wa Marekani, Donald Trump, imependekeza kufutiliwa mbali kwa mfuko wa ufadhili wa operesheni za kulinda amani za umoja wa Mataifa, ikidai ni kutokana na kushindwa kwa operesheni za Mali, Lebanon na DRC.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na nyaraka zilizoonwa na shirika hilo, Washington inasema ujumbe wa kulinda amani nchini Mali, Lebanon na DRC umeshindwa kufikia malengo.
Marekani ni mojawapo wa wafadhili wakubwa katika ujumbe wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa duniani ikifuatiwa na China.
Kwa sasa bajeti mpya kuhusu ujumbe huo ni lazima iidhinishwe na bunge la Congress ambapo wabunge watakuwa na jukumu la kuamua iwapo watarejesha ufadhili kama ilivyokuwa awali au wataridhia mapendekezo ya Ofisi ya bajeti kukata ufadhili.
Katika muhula wa kwanza wa rais Trump, alipendekeza kupunguzwa kwa robo tatu ya bajeti kuhusu masuala ya kidiplomasia na misaada, pendekezo ambalo lilikataliwa na bunge la Congress.