Marekani yajipanga kutuma idadi kubwa zaidi ya wanajeshi na zana za kivita Asia Magharibi

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza mpango wa kutumewa wanajeshi zaidi wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi.

Msemaji wa Pentagon, Pat Ryder, amesema: Pentagon inapanga kujizatiti na kuwepo zaidi kijeshi katika eneo la Asia Magharibi kwa kutuma ndege za udondoshaji mabomu, ndege za kivita pamoja na manowari.

Msemaji wa Pentagon pia amesema kuwa,  Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ameamuru kutumwa ndege kadhaa za kimkakati za udondoshaji mabomu aina ya B-52 Stratofortress, kikosi cha usindikizaji ndege za kivita, ndege za kujaza mafuta na manowari za mashambulizi huko Asia Magharibi, na akaongezea kwa kusema, kuwasili wanajeshi wapya wa Kimarekani katika eneo hilo kutaanza katika miezi ijayo, sambamba na kuanza kuondoka Asia Magharibi na kurejea Marekani manowari ya kubebea ndege ya USS Abraham Lincoln na msafara wa manowari zinazoandamana nayo.

Pat Ryder

Manowari ya kubebea ndege za kivita ya USS Abraham Lincoln na manowari tatu za mashambulizi za Jeshi la Wanamaji la Marekani ambazo zinaongozwa na kikosi kazi cha operesheni za mashambulio cha manowari hiyo ya kubebea ndege za kivita zimepangiwa kuondoka Asia Magharibi na kurejea katika bandari yao ya San Diego katikati ya mwezi  Novemba.

Kutokana na kuhofia jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran kwa uchokozi wowote unaofanywa na utawala wa Kizayuni, Rais Joe Biden wa Mareani alitangaza katika barua yake kwa Bunge la  nchi hiyo, Kongresi kwamba jeshi la Marekani litaendelea kubakia katika eneo la Magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati).