Marekani imeitaka nchi ya Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake katika ardhi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa amani, vyanzo vya kidiplomasia vimesema.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali ni kuwa Marekani ambayo inaendeleza mpango wa amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo itahitaji Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo kabla ya pande hizo mbili, DRC na Rwanda yenyewe kutia saini makubaliano ya amani.
Sharti hilo la Marekani huenda likaikasirisha Kigali ambayo imekuwa ikitetea uwepo wake huko Congo kutokana na kile serikali ya Kigali inasema makundi yenye silaha nchini Kongo ni tishio la kudumu kwa usalama wake, na eneo la maziwa makuu.
Serikali ya Rais Donald Trump ambayo inasimamia mazungumzo ya amani ya DRC imewekeza mabilioni ya dola kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo lenye utajiri wa madini.
Rasimu ya mkataba wa amani iliyopendekezwa katika mikutano ya Doha na Marekani imeonyesha kwamba sharti mojawapo lililoorodheshwa kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa amani huko mashariki mwa DRC, ni kwamba Rwanda inatakiwa kuwaondowa wanajeshi wake, silaha na vifaa vyake vyote huko Kongo.
Sharti hili la kuitaka Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake huko DRC pia lilitolewa hivi majuzi katika mkutano wa kilele wa 26 viongozi wakuu wa jumuia ya Nchi za Afrika ya kati ECCAS uliofanyika huko Malabo Equatorial Guinea mwishoni mwa juma lililopita na ambao walisisitiza kuwa lazima mipaka ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo iheshimiwe.