
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio hatahudhuria mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi tajiri na zinazoendelea unaoanza leo Alhamisi Februari 20 baada ya kukosoa sera za nchi mwenyeji Afrika Kusini kuwa ni chuki dhidi ya Marekani.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Badala yake, Rubio alirejea Marekani siku ya Jumatano baada ya ziara yake ya kwanza Mashariki ya Kati kama mwanadiplomasia mkuu wa Marekani, na baada ya kuongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo na Urusi nchini Saudi Arabia kuhusu vita vya Ukraine.
Rubio alizungumza na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ili kuwafahamisha mara baada ya mkutano wa Jumanne na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, Wizara ya Mambo ya Nje imesema.
Wanadiplomasia wakuu wa Ulaya, pamoja na Lavrov na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, wote wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa G20 mjini Johannesburg, huku Marekani ikiwakilishwa na wajumbe wa ngazi ya chini.
Mkutano wa G20 kwa kawaida ungekuwa fursa kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani kushawishi uungwaji mkono kwa misimamo ya Marekani, hasa mwanzoni mwa utawala mpya.
Wachambuzi wanasema kutokuwepo kwa Rubio kunaonyesha kutojali kwa utawala wa Trump kwa mashirika yanayokuza ushirikiano wa kimataifa, lakini Rubio pia alikataa moja kwa moja vipaumbele vya Afrika Kusini kwa urais wake wa G20. Waandaji walichagua “mshikamano, usawa, uendelevu” kama mada ya G20 ya mwaka huu.
Afrika Kusini, taifa la kwanza la Afrika kushika wadhifa wa urais wa kundi hilo, inasema itajaribu kuendeleza maslahi ya nchi maskini, ikiwa ni pamoja na kufadhili madeni na kuzisaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo mataifa yanayoendelea yanazitaka nchi tajiri kulipa zaidi.
Rubio aliandika kwenye mtandao wa X mwezi huu kwamba pia hatahudhuria mkutano mkuu wa G20 huko Johannesburg mmwezi Novemba, akisema Afrika Kusini inatumia mkutano huo kukuza utofauti, usawa na mifumo ya ujumuishi, “kwa maneno mengine: DEI na mabadiliko ya tabianchi.”
“Kazi yangu ni kuendeleza masilahi ya kitaifa ya Marekani, sio kupoteza dola za walipa kodi au kuchochea chuki dhidi ya Marekani,” Rubio aliandika.
Uamuzi wa Rubio wa kutohudhuria mkutano wa G20 pia unasisitiza kuzorota kwa uhusiano wa Marekani na Afrika Kusini, mojawapo ya washirika wake wakubwa wa kibiashara barani Afrika.
Rais Donald Trump alitia saini agizo la kiutendaji mapema mwezi huu kuhitimisha misaada na usaidizi wa Marekani kwa Afrika Kusini kuhusu sheria ya ardhi anayosema inawabagua wazungu wachache nchini humo. Agizo hilo pia linaitaja sera ya mambo ya nje ya Afrika Kusini kuwa dhidi ya Marekani na inakosoa kesi inayoendelea dhidi ya Israeli ya mauaji ya halaiki huko Gaza mbele ya Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa, pamoja na kile inachokiona kuwa ukaribu wa nchi hiyo na Chama cha Kikomunisti cha China.
Afrika Kusini inatazamiwa kukabidhi urais wa G20 kwa Marekani mwishoni mwa mwaka huu, na nchi hizo mbili zinatarajiwa kufanya kazi pamoja chini ya itifaki za G20.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola alisema siku ya Jumatano kwamba Marekani itawakilishwa mjini Johannesburg wiki hii “kwa namna fulani au nyingine” na kusisitiza kwamba uamuzi wa Rubio “sio Marekani kususia kikamilifu kikao cha G20 kinachofanyika Afrika Kusini” na Marekani.
Wachambuzi wa Afrika wanasema bado wanaona njia kwa G20 kufanya maendeleo chini ya urais wa Afrika Kusini, hata kama nia ya Marekani ni ndogo. EU, Urusi na China zimeonyesha kuunga mkono uongozi wa Afrika Kusini wa G20.
“Hakuna mtu anataka kuwa upande mbaya wa Marekani,” alisema Oscar van Heerden, mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Diplomasia na Uongozi wa Afrika cha Chuo Kikuu cha Johannesburg. “Lakini nadhani kila mtu pia anatambua kwamba kinachochochea sera ya nje ya Marekani sio lazima kuwa kile kinachoongoza sera ya kigeni ya Umoja wa Ulaya au wanachama wengine wa G20. “
Washirika wa Ulaya wana wasiwasi wao kuhusu ushirikiano wa siku zijazo na utawala wa Trump baada ya kutengwa na uamuzi wake wa kufanya mazungumzo ya pande mbili wiki hii na Urusi.
“Uhusiano wa pande nyingi kwa sasa uko chini ya tishio,” mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, akiwa nchini Afrika Kusini, amesema. “Lazima pia tuchukue fursa hii kuendeleza zaidi mfumo wa kimataifa ili ujumuishe zaidi kwa nchi zote za ndani.