Marekani: Utawala wa Trump watangaza kufuta 83% ya mipango ya maendeleo ya USAID

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ametangaza siku ya Jumatatu, Machi 10, 2025, kwamba 83% ya mipango ya shirika la maendeleo la USAID, ambayo inawakilisha sehemu kubwa ya misaada ya kibinadamu duniani, itafutwa.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Baada ya mapitio ya wiki sita, tunafuta rasmi 83% ya programu za USAID,” mkuu wa diplomasia ya Marekani ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X, akimaanisha “makumi ya mabilioni ya dola” yaliyotumiwa bila ya lazima, bila kutoa takwimu sahihi zaidi. “Kwa makubaliano na Barazala la Congress, tunataka asilimia 18 ya programu ambazo zimebakia (takriban 1,000) sasa zisimamiwe kwa ufanisi zaidi na Wizara ya Mambo ya Nje,” ameongeza.

Wizara ya Mambo ya Nje, ambayo inasimamia USAID, ilitangaza Februari 26 kuwa inalenga kupunguza asilimia 92 ya ufadhili wa mpango wa shirika hilo, kuokoa dola bilioni 54.

USAID imekuwa ikisimamia 42% ya misaada ya kibinadamu duniani

Rais Donald Trump alitia saini agizo la utendaji baada ya kurejea Ikulu ya White House mnamo Januari 20, na kuagiza kusitishwa kwa siku 90 kwa msaada wa kigeni wa Marekani wakati akifanya mapitio kamili ili kutathmini uhalali wake na sera anazokusudia kufuata, ikiwa ni pamoja na kupiga vita programu zinazohimiza uavyaji mimba, kupanga uzazi, na utofauti na ushirikishwaji.

Uamuzi huo umesababisha mshtuko na hisia kwa mashirika ya kutoa misaada na ndani ya USAID, shirika huru lililoundwa mnamo mwaka 1961 na ambalo hadi sasa linasimamia bajeti ya kila mwaka ya dola bilioni 42.8, au 42% ya misaada ya kibinadamu iliyotolewa ulimwenguni kote. Mashirika kadhaa duniani yanasema tayari yanakabiliwa na athari kufuatia  hatua ya Marekani ya kusitishwa kwa misaada ya kibinadamu, iwe kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI nchini Afrika Kusini au Kenya, au jikoni za supu nchini Sudani, nchi iliyoharibiwa na vita.

Matokeo ya mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani

Matokeo ya mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani yanapaswa pia kuhisiwa haraka. Mnamo mwaka 2024, kwa zaidi ya euro bilioni kumi, msaada wa Marekani katika mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani uliwakilisha karibu sehemu ya kumi ya ufadhili wa kimataifa. USAID pekee ilitoa theluthi moja ya kiasi hicho kupitia mamia ya programu. Hizi zitakuwa kati ya za kwanza kufutwa baada ya tangazo la Marco Rubio, kwani fedha hizi zimetambuliwa kuwa lengo kuu tangu mwanzo.

Mabilioni yaliyosalia yanasimamiwa na zaidi ya mashirika kumi na mbili, ambayo yanasambaza ruzuku, mikopo, na ufadhili wa maendeleo. Ushiriki katika fedha za kimataifa pia uko chini ya tishio. Marekani, kwa mfano, imefuta ahadi ya euro bilioni nne kwa Mfuko wa Kijani kwa ajili ya Tabianchi. Kwa kuzingatia kufutwa huku, mchango wa Marekani kwa hazina hii sasa ni mdogo kuliko ule wa Sweden, ambao uchumi wake ni mdogo mara 50, vinaripoti vyombo vya habari vilivyobobea vya Carbon Brief.

Kiwango cha kujitolea kiko mbali na jukumu la Marekani la ongezeko la joto duniani. Nchi tajiri zaidi ulimwenguni pia ndiyo ambayo kihistoria imetoa gesi chafu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *