Marekani, Ukraine kukutana tena wiki ijayo Saudi Arabia

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine yatafanyika Saudi Arabia wiki ijayo, akieleza matumaini kwamba utakuwa mkutano wenye maana.

Kwa mujibu wa BBC, kiongozi huyo wa Ukraine, ambaye atakuwa katika ufalme huo wa Ghuba, hatashiriki katika mazungumzo hayo, ambapo mazungumzo hayo ya Saudi Arabia yatakutanisha timu maalumu kutoka Marekani na Ukraine kujadili mustakabali wa vita ya Russia na Ukraine. Zelensky alisema Kyiv inapambana kufikia amani ya haraka na ya kudumu.

Mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Steve Witkoff, amesema timu ya Marekani ilitaka kujadili mfumo wa amani kujaribu kumaliza vita vya Russia na Ukraine.

Ijumaa iliyopita, Zelensky na Trump walizozana hadharani katika Ikulu ya White House ambapo Trump alisema Zelensky hakuwa tayari kumaliza mapigano.

Marekani baadaye ikatangaza kusitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kusimamisha kushirikiana kwenye taarifa za kijasusi.

Rais wa Ukraine ameonyesha majuto kuhusu tukio hilo na kujaribu kurekebisha uhusiano na Marekani ambayo ndiyo inayotoa msaada mkubwa wa kijeshi wa nchi hiyo.

Witkoff alisema Alhamisi iliyopita, Trump alipokea barua kutoka kwa Zelensky iliyojumuisha kuomba msamaha na kuonyesha hisia ya shukrani. “Tunatumaini tutarejesha mambo kwenye mstari na Waukraine, na kila kitu kitaanza tena,” alisema Witkoff.

Zelensky amekuwa chini ya shinikizo kubwa la Marekani kufanya makubaliano kabla ya mazungumzo yoyote ya amani, wakati Rais wa Ukraine amekuwa akishinikiza dhamana thabiti za usalama kwa Kyiv.

Zelensky alitangaza mazungumzo ya Marekani na Ukraine nchini Saudi Arabia katika mfululizo wa machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kuhudhuria mkutano wa dharura wa Alhamisi mjini Brussels ambapo viongozi wa Umoja wa Ulaya waliidhinisha mipango ya kuongeza matumizi ya ulinzi.

“Timu za Ukraine na Marekani zimeanza tena kazi, na tuna tumaini kwamba wiki ijayo tutakuwa na mkutano wenye maana.

“Ukraine imekuwa ikitafuta amani tangu wakati wa kwanza wa vita, na tumekuwa tukisema kila wakati kwamba vita vinaendelea tu kwa sababu ya Russia,” aliandika kwenye X.

Zelensky alihimiza jumuiya ya kimataifa kuweka shinikizo zaidi kwa Russia ili ikubali hitaji la kumaliza vita. Russia ilianzisha uvamizi kamili wa Ukraine Februari 2022 na sasa inadhibiti takriban asilimia 20 ya eneo la Ukraine.