Marekani, Ufilipino zaimarisha muungano kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi

Vikosi vya anga vya Ufilipino na Marekani vimeanza mazoezi ya pamoja ya kijesi siku ya Jumatatu yenye lengo la kuimarisha uratibu wa utendaji kazi na “zuio la kimkakati,” maafisa katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia wamesema.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mazoezi hayo yanafuatia miezi kadhaa ya mvutano kati ya Beijing na Manila katika Bahari ya Kusini ya China. “Kuboresha utayari wa mapambano na ufanisi wa misheni ya pamoja” itakuwa kiini cha mazoezi ya operesheni iliyopewa jina la “Cope Thunder,” Mkuu wa Jeshi la Wanahewa la Ufilipino Arthur Cordura amesema leo Jumatatu, Aprili 7, wakati wa hafla ya uzinduzi.

Manila na Washington zimeimarisha ushirikiano wao wa kiulinzi tangu Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos aingie madarakani mwaka 2022, akipinga vikali madai ya Beijing katika Bahari ya Kusini ya China. China inadai umiliki wa visiwa vingi na miamba katika bahari hii, pamoja na maji na visiwa karibu na pwani ya nchi kadhaa jirani.

Marekani ilitangaza wiki iliyopita kuwa imeidhinisha uuzaji wa ndege 20 za kivita za F-16 kwa Ufilipino, ingawa Manila imesema mkataba huo “bado upo kwenye mazungumzo.” “Kasi ya muungano wetu inaongezeka,” Afisa wa Marekani mwenye cheo cha Meja Jenerali katika jeshi la Marekani Christopher Sheppard amesema katika hafla hiyo.

Mazoezi katika eneo la Ufilipino lililo karibu zaidi na Taiwan “Cope Thunder,” ambayo yanaendelea hadi Aprili 18, yanalenga kuboresha “uwezo wa vita usiolinganishwa,” ikimaanisha vita kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji, uratibu wa operesheni na zuio la kimkakati, kulingana na Jeshi la Anga la Ufilipino. Mazoezi hayo yamepangwa kufanyika kaskazini mwa Kisiwa cha Luzon, eneo la Ufilipino lililo karibu zaidi na Taiwan. Mazoezi makubwa ya anga, ardhini na baharini kati ya Marekani na Ufilipino, yanayojulikana kama “Balikatan,” pia yamepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Aprili.

Wiki iliyopita, wakati China ikifanya mazoezi makubwa ya kijeshi ya kuiga kizuizi cha Taiwan, mkuu wa jeshi la Ufilipino Romeo Brawner alisema kuwa vikosi vya nchi hiyo “bila shaka” vitahusika katika tukio la uvamizi wa kisiwa hicho, ambacho Beijing inadai. Manila baadaye ilidai kuwa maoni hayo yalikuwa yakimaanisha kutumwa kwa wanajeshi kwa minajili ya kuwaejesha nyumbani wafanyakazi wa Ufilipino kutoka Taiwan ikiwa kutatokeamzozo.

Mkataba ulioimarishwa wa ushirikiano wa kiulinzi na Washington unavipa vikosi vya Marekani ufikiaji wa vituo tisa nchini humo. Katika ziara ya hivi majuzi mjini Manila, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth alisema Washington “inaongeza maradufu juhudi zake” ili kuimarisha muungano wake na visiwa hivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *