
Tukio kubwa la soka ambalo linasubiriwa kwa hamu mwezi huu ni mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu baina ya Yanga na Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 8.
Ni mechi ambayo ina maana kubwa katika kuamua mbio za ubingwa baina ya timu hizo mbili kutegemea na msimamo wa ligi ulivyo kwa hivi sasa.
Tofauti ya pointi nne tu ndio inayozitofautisha timu hizo mbili kwa sasa hivyo ushindi kwa Yanga maana yake utaifanya iongeze pengo la pointi kati yake na Simba kufikia saba.
Lakini kwa Simba ikiibuka na ushindi itapunguza pengo la pointi baina yake na Yanga kubakia moja huku yenyewe ikibaki na faida ya kuwa na mchezo mmoja mkononi.
Ikumbukwe kwamba Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 58 ambazo imekusanya katika michezo 22 na Simba ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 ambazo imevuna katika mechi 21.
Hakuna namna ambayo unaweza kuelezea mechi baina ya timu hizo mbili zaidi ya homa ya nchi kwa vile Tanzania nzima husimama kwa muda kupisha dakika 90 za mchezo huo.
Ni ndoto na shauku ya kila mchezaji wa timu hizo kucheza mechi yenye mvuto na msisimko mkubwa kama hiyo kwani huwapa fursa ya kuandika historia na wengine kuvuna kiasi kikubwa cha fedha iwapo timu yao inapoibuka na ushindi.
Hapana shaka ni mchezo ambao utateka hisia za mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla na kama ilivyozoeleka pindi timu hizo zinapokutana, baadhi ya shughuli husimama kwa muda kupisha tukio hilo kubwa kisoka nchini.
Hii ni kwa sababu ya ukubwa na thamani ambazo klabu hizo mbili kongwe zinao na hilo ni zao la ukongwe wa umri na mafanikio makubwa ambayo Yanga na Simba zimepata tangu zilipoanzishwa kulinganisha na klabu nyingine hapa nchini.
Hizo ndio timu mbili ambazo zimefanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Yanga inaongoza kwa kutwaa taji mara 30 huku Simba yenyewe ikiwa imeibuka bingwa wa ligi mara 22.
Mafanikio ya timu hizo mbili hayajaishia katika Ligi Kuu Tanzania Bara pekee bali hata kimataifa kwani ndio zinafukuzana pia katika kutwaa ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ambapo Simba ni kinara ikiwa imechukua Kombe mara sita huku Yanga ikitwaa ubingwa mara tano sawa na AFC Leopards ya Kenya.
Na mvuto na msisimko wa mechi baina ya timu hizo mbili ndio umefanya itajwe kuwa miongoni mwa mechi kubwa za watani wa jadi (derbies) barani Afrika hasa ikichagizwa na idadi kubwa ya mashabiki ambao hujitokeza uwanjani kwenda kushuhudia mechi hiyo.
Lakini pia namba ya wafuatiliaji wa pambano linalokutanisha Yanga na Simba ni sababu nyingine ambayo imefanya wadau wa mpira wa miguu kuiweka katika kundi la mechi kubwa za watani wa jadi katika bara hili la Afrika.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, mechi ya Yanga na Simba inashika nafasi ya tano katika orodha ya mechi 10 bora za watani wa jadi barani Afrika.
Nafasi ya kwanza inashikiliwa na mechi ya watani wa jadi ya jiji la Cairo, Misri ambayo hukutanisha timu za Al Ahly na Zamalek wakati nafasi ya pili ni ile ya jiji la Casablanca, Morocco ambayo hukutanisha timu za Raja Casablanca na Wydad Casablanca.
Mechi ya watani wa jadi inayoshikilia nafasi ya tatu ni ile ya Soweto ambazo hukutanisha timu mbili kubwa zinazotoka kitongoji cha Soweto, Johannesburg, Afrika ya Kusini ambazo ni Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Na mchezo bora wa watani wa jadi unaoshika nafasi ya nne barani Afrika kabla ya mechi ya Simba na Yanga ni ule wa jiji la Tunis, Tunisia ambao hukutanisha miamba miwili ya soka Afrika inayotokea jijini humo, Esperance na Club Africain.
Kitendo cha mechi baina ya Simba na Yanga kushika nafasi ya tano katika orodha ya mechi 10 za watani wa jadi Afrika, kinafanya ufuatiliwe zaidi katika maeneo tofauti ndani na nje ya bara la Afrika.
Hii ni fursa kwa wachezaji kujiweka sokoni kwani timu, mawakala na maskauti mbalimbali wa soka wanapata nafasi ya kuwatazama na kujiridhisha juu ya ubora wao.
Fursa hiyo haipaswi kuishia kwa wachezaji tu bali hata kwa waamuzi ambao wamepangwa kuichezsha, wanatakiwa kujitahidi kutafsiri vyema sheria 17 za mpira wa miguu ili nao waweze kushawishi mamlaka kubwa zinazosimamia soka duniani, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) na lile la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwapa nafasi pindi kunapokuwa na mechi za kimataifa za mashindano mbalimbali.