Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame, hapo jana wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja ikiwa ni mara ya kwanza tangu waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Kigali kuteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Congo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi ya Qatar, ambayo ilikuwa mpatanishi katika mazungumzo yaliyofanyika mjini Doha, viongozi hao wamekubaliana kimsingi “kusitishwa mara moja kwa mapigano” mashariki mwa DRC.
Taarifa imeongeza kuwa rais Tshisekedi na Kagame, walikubaliana kuhusu haja ya kuendelea na majadiliano yaliyoanzishwa huko Doha ili kuweka misingi imara ya amani ya kudumu,” ilisema taarifa hiyo.
DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kutuma silaha na wanajeshi kuwasaidia waasi wa M23 jambo ambalo Rwanda imeendelea kukanusha.
Mazungumzo haya yamefanyika baada ya wawakilishi wa M23 kujiondoa katika mazungumzo kati yake na serikali ya Kinshasa nchini Angola, uamuzi waliouchukua baada ya Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa kundi akiwemo Bertrand Bisimwa.
Mzozo mashariki mwa DRC uliongezeka mwezi Januari wakati waasi waliposonga mbele na kuuteka mji wa kimkakati wa Goma, ukifuatiwa na Bukavu mwezi Februari.
Kwa mujibu wa ripoti za umoja wa Mataifa, waasi hao wanaungwa mkono na takriban wanajeshi 4,000 wa Rwanda.