Maradhi ya Papa Francis yakatisha ziara ya Mfalme Charles Vatican

Mfalme Charles na Malkia Camilla wa Uingereza wamelazimika kukatisha ziara yao ya kiserikali waliyopanga kuifanya Vatican na kukutana na Papa Francis mwezi ujao.

Jana Machi 25, 2025 Ikulu ya Buckingham ilitangaza kuwa ziara hiyo imeahirishwa kwa makubaliano ya pande zote kutokana na ushauri wa kitabibu aliopewa Papa Francis wa kupumzika muda mrefu, baada ya kulazwa kwa wiki takriban tano.

Papa Francis aliruhusiwa kutoka hospitali alikolazwa kwa maradhi ya nimonia, Jumapili Machi 23, 2025.

Katika taarifa  ya Ikulu ya Buckingham ilieleza: “Ziara ya Kitaifa ya Mfalme na Malkia kwenda Vatican imeahirishwa kwa makubaliano ya pande zote mbili, kwani ushauri wa kimatibabu sasa umependekeza kuwa Papa Francis anatakiwa kupata muda mrefu wa kupumzika, wanatazamia kumtembelea, mara tu atakapopata nafuu.”

Papa Francis alivyorejea nyumbani

Machi 23, 2025 katika hali ya udhaifu, Papa Francis alionekana akiwa amebebwa kwenye gari maalumu kutoka Hospitali ya Gemelli mjini Roma, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa nimonia, hali iliyomlaza hospitalini kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea tangu alipochaguliwa kuwa Papa mwaka 2013.

Shirika la Habari la Reuters liliripoti kuwa Papa Francis aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupona ugonjwa huo ambao ulikuwa tishio kwa uhai wake.

Alipokuwa akirejea nyumbani, alifanya ziara fupi katika basilika anayoiabudu, kabla ya kuanza mapumziko ya miezi miwili aliyoagizwa na madaktari ili kupata ahueni kamili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *