Mapya yaibuka wanasheria wa Kenya kuzuiwa Tanzania kumtetea Lissu

Mapya yaibuka wanasheria wa Kenya kuzuiwa Tanzania kumtetea Lissu

Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema mawakili kutoka nchini Kenya waliozuiwa kuingia nchini kumtetea Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu hawana leseni ya kufanya shughuli za uwakili Tanzania.

Wakati Dk Ndumbaro akisema hayo, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema kinachoonekana kwenye tukio hilo ni kwamba Serikali haikupewa taarifa sahihi kuhusiana na ujio wa mawakili hao.

Dk Ndumbaro alikuwa akizungumzia tukio la kuzuiwa kuingia nchini kwa wanasheria kutoka Kenya akiwemo Martha Karua, Lynn Ngugi, Gloria Kimani, na Jaji Mkuu mstaafu, Dk Willy Mutunga, waliodaiwa kuwa walikuja kushiriki katika kesi ya Lissu.

Hata hivyo, Jaji Mkuu mstaafu David Maraga wa Kenya pamoja na mwanasheria mmoja kutoka Comoro walifanikiwa kuingia nchini na kuhudhuria kesi hiyo.

Dk Ndumbaro amesema walichokuwa wanakuja kukifanya hapa nchini ni uvunjifu wa sheria za Tanzania, jambo ambalo halikubaliki.

“Rais (Rais Samia Suluhu Hassan) aliongea kistaarabu sana, sisi wengine kuna siku ustaarabu huwa tunauacha nyumbani. Kuna ndugu zetu Wakenya walikuja wakazuiwa pale airport (uwanja wa ndege) wanasema wamekuja kwenye kesi ya Tundu Lissu kusimamia haki za binadamu.

“Kwa uelewa wangu wale hawana leseni ya kufanya shughuli za uwakili Tanzania, kwa hiyo hiki wanachokuja kukifanya ni uvunjifu wa sheria zetu. Lakini kule kwao yamewashinda, nyumba yao inawaka moto unataka kuuzima wa jirani? Huu ni unafiki,” amesema na kuongeza;

“Sisi Watanzania hatutaki unafiki, kwenye eneo la haki za binadamu tupo vizuri na naungana na mheshimiwa Rais kwenye kauli yake ya jana,” amesema Ndumbaro.

Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Mei 20, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita jijini Dodoma.

Amesema Tanzania ina mafanikio kwa kuwa na chombo cha kisheria kinachosimamia haki za binadamu ambacho kimepata daraja A toka kwa waangalizi mahususi wa kimataifa.

“Nchi inafanya vizuri, kwa hiyo tuachanane na propaganda zinazoletwa na watu wasioitakia mema nchi,” amesema.

Pia, amesema mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoundwa ya kushughulikia masuala ya haki jinai nchini yameanza kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya, ikiwemo kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.

Mwabukusi atoa kauli

Kwa upande wake, Boniface Mwabukusi amesema kinachoonekana kwenye tukio hilo ni kwamba Serikali haikupewa taarifa sahihi kuhusiana na ujio wa mawakili hao.

“Nadhani waziri hakupewa taarifa sahihi kwa sababu hoja ya waziri ni sahihi kwa muktadha huo, lakini si sahihi kwa muktadha uliotumika kuwazuia hao waliokuja sasa, kwa sababu hao waliokuja hawakuja kufanya kazi ya uanasheria, walikuwa wanakuja kufanya observation (uangalizi), yaani kumtembelea mwanasheria au mwanaharakati mwenzao ambaye yupo katika maswahibu.

“…Kupata leseni ni pale unapohitaji kuwasiliana rasmi na mahakama na utaapishwa kama wakili unayetaka kufanya kazi nchini,” amesema.

Amefafanua kuwa hakuna sheria inayomzuia mtu kusikiliza kesi au kuingia mahakamani kama mtazamaji, akisisitiza kuwa kigezo cha kuwa na cheti au leseni kinahitajika kwa wale tu wanaotaka kutoa huduma za kisheria mahakamani.

Akizungumzia kauli ya waziri kuhusu watu hao kutoka nje ya nchi kutokuwa na leseni, Mwabukusi amesema huenda waziri huyo alimaanisha suala la kufanya kazi ya uwakili, si kushiriki kwa njia ya usikilizaji wa kesi.

“Waziri alikuwa anazungumzia suala tofauti kabisa na lililowaleta hawa mawakili kutoka Kenya na Uganda. Kwa sababu hawakuja kufanya kazi za uwakili, kuja kusikiliza kesi si kosa hata kidogo,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa kwa mujibu wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, haki ya wanachama kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine iko wazi, hivyo kisheria hawakufanya kosa.

“Kama kuna mtu ametenda kosa, basi liangaliwe ni kosa gani, lakini kama ni kwenda Kisutu tu kusikiliza kesi, hilo siyo kosa,” amesema.

Wakati huo huo, Katibu wa Itikadi, Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema Tanzania ni nchi huru yenye mamlaka kamili, hivyo ina uwezo wa kuamuru mgeni gani aingie nchini na nani asiingie.

Makalla ameeleza hayo akikazia maelezo yaliyotolewa jana na Rais Samia aliyevitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutotoa nafasi kwa wanaharakati kutoka mataifa mengine wanaokuja kuingilia mambo ya ndani ya nchi na kuchochea vurugu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *