Dar es Salaam. Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Mohamedi Mnemwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili katika kitengo cha Mifupa Moi kufuatia kipimo cha CT Scan kuonyesha damu imevilia kwenye ubongo.
Hali hiyo imetokea baada ya wikiendi iliyopita bondia huyo kuzimia baada ya kupigwa kwa Technical Knockout ya raundi ya tatu katika pambano la raundi nne dhidi ya Ally Sewe ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa Mrina, Tip top, Manzese, Dar.
Mnemwa ambaye mchana wa juzi Jumatatu, alifanyiwa kipimo hicho katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke hali iliyolazimu kuandikiwa rufaa ya kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi na kuelezwa atalazwa kwa siku tatu.
Kwa mujibu wa mtandao wa kuhifadhi taarifa za mabondia duniani, boxrec unaonyesha pambano hilo ndiyo lilikuwa la kwanza kwa Mnemwa na mpinzani wake katika ngumi za kulipwa, akipewa namba ya usajili 1303950 kwenye uzani wa Fly.
Mwananchi ambalo lilikuwepo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke wakati bondia huyo anafikishwa hapo, limeshuhudia bondia huyo akipelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kufanyiwa kipimo hicho ambacho kimegundua tatizo la kuvilia damu kwenye ubongo.
Daktari wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini, TPBRC, Dk Hadija Hamisi alisema kuwa tayari mgonjwa huyo ameshapata kipimo cha CT Scan na amegundulika na tatizo hilo kwenye ubongo hali iliyopelekea kupewa rufaa ya kupelekwa Muhimbili.
“Mgonjwa ameshafanyiwa kipimo cha CT Scan na amegundulika kuwa damu imevilia kwenye ubongo kwa sababu kipimo kinaonyesha fuvu limepata mpasuko ambalo limesababisha tatizo hilo.
“Hapa tumepata rufaa ya kupelekwa Muhimbili katika kitengo cha Mifupa Moi kwa ajili ya kupata vipimo zaidi, lakini kama unavyomuona mgonjwa bado hali yake siyo nzuri, analamikia kuumwa na kichwa pamoja na macho,” alisemaHadija.
Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta mmoja kati ya wauguzi wa bondia huyo ambaye ni nahodha wa Gym ya Mumbamba Boxing Zone, Khalid Manjee alisema wamepokelewa vizuri baada ya kufika Moi huku mgonjwa akitakiwa kulazwa kwa muda wa siku tatu kwa ajili ya matibabu.
“Tumepokelewa hapa na tumepewa taarifa kuwa mgonjwa anatakiwa kulazwa kwa siku tatu ili afanyiwe vipimo vizuri,” alisema Manjee.
Ikumbukwe Desemba, mwaka jana bondia Hassan Mgaya alifariki katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanyamala ikiwa ni muda mchache tangu apewe rufaa ya kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuatia kupigwa kwa Knockout katika pambano lake dhidi ya Paul Elias.