Shinyanga. Kuporomoka kwa kifusi katika mgodi unaomilikiwa na kikundi cha Hapa Kazi Tu, Mwakityolo mkoani Shinyanga, kumepoka uhai wa watu sita na kuwajeruhi 17 kwa mujibu wa taarifa rasmi ya uokozi hadi leo saa 12:00 jioni.
Hadi taarifa ya mwisho ya uokozi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga inayotolewa leo, inadaiwa watu 20 ndiyo waliokuwepo katika eneo hilo.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Mei 17, 2025, wakati wachimbaji hao walipokuwa wakiendelea na kazi katika mgodi huo wa dhahabu.
Akizungumzia hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thomas Majuto, amesema shughuli ya uokoaji imekamilika leo mchana, huku miili sita ikiopolewa na majeruhi 11, hivyo jumla ya watu 17 wamepatikana.

Katika maelezo yake, Majuto amefafanua sababu ya wachimbaji hao kutoandikishwa kwenye kitabu cha kumbukumbu ni kuingia katika eneo hilo kinyume na utaratibu.
“Hawakuwa wachimbaji rasmi wa eneo lile, bali ni wavamizi wanaopita nyakati za usiku kwa lengo la kuokota mawe ya dhahabu kinyume na utaratibu.
“Hao ni wale waliopewa jina lisilo zuri sana, sitaki kulitaja, wanaopita kwenye maeneo yenye leseni hasa nyakati za usiku, wakati wamiliki wakitoka kwa lengo la kuokota mawe ya dhahabu, kwa hiyo wanakuwa hawajaandikishwa,” amesema Majuto.
Amewataka wachimbaji kuzingatia utaratibu wa kiusalama hasa wa kuingia na kutoka kwenye migodi, ikiwa ni pamoja na kuandikishwa kwenye kitabu cha kumbukumbu.
“Tusitumie sana hisia za kupata fedha tukasahau uhai wetu hasa kwenye maeneo hatarishi. Tutoe taarifa kwa wenye migodi au mamlaka za Serikali kuhusu maeneo hayo ili kuokoa uhai wetu,” amesema.
Awali, akitoa taarifa ya tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amesema kati ya majeruhi 11 wanaopatiwa matibabu, mmoja ameruhusiwa baada ya afya yake kuimarika na wengine wanaendelea kutibiwa.
Ameeleza shughuli ya uokoaji ilifanywa na askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoani humo kwa kushirikiana na wananchi.
Hata hivyo, amesema idadi ya watu wanaotajwa kuwepo katika eneo lililoporomoka haijathibitishwa.
“Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchimbaji madini nchini, kila mtu anayeingia ndani ya mgodi anapaswa kuandikishwa jina, haijafahamika mara moja ni kwa nini imekuwa vigumu kujua idadi halisi ya walioingia mgodini siku ya ajali,” amesema.
Mchimbaji katika mgodi huo, George Bujiku, akizungumza na Mwananchi, ameiomba Serikali fanye ukaguzi wa mara kwa mara kwenye migodi midogo kwani kunakuwa na changamoto ndogondogo zinazosababisha majanga ya aina hiyo.
“Nilichokiona katika ukataji wao walivyokata hili gema inaonekana lilikuwa limeoza huko juu ni kama lilijiegesha, sasa wachimbaji wakawa wanachimba kwa chini, jana kukatokea mtikisiko wa skaveta lililokuwa linachoronga eneo lingine, hivyo kifusi kikadondoka,” amesema.

Kwa upande wa Michael Mzibamziba, amesema Serikali ifanye uchunguzi zaidi kwenye eneo la ajali ili kuhakikisha waathirika wote wanatolewa chini ya kifusi, kwani wapo jamaa zake aliokuwa akizungumza nao kwa njia ya simu, lakini sasa hawapatikani.
“Hiki kitalu tunavyokijua, wachimbaji wanaofika hapa asubuhi ni wengi. Hao waliotoka hapa ni wachache japokuwa hatujui idadi kamili, ila tulichokuwa tunakiomba hiyo sehemu waliyoakia ifukuliwe wangeifanyia uchunguzi vizuri ili tujihakikishie kama kuna waliobaki pale tuwatoe,” amesema.
Hilo sio tukio la kwanza la watu kufukiwa na kifusi mgodini nchini, iliwahi kutokea Januari 13, 2024, katika mgodi mdogo wa dhahabu wa Ng’alita, wilayani Bariadi katika Mkoa wa Simiyu.
Katika tukio hilo, wachimbaji 22 walipoteza maisha baada ya kuingia katika eneo lililokuwa limezuiwa kutokana na mvua kubwa na kufukiwa na kifusi.
Tukio linalofanana na hilo, lilitokea Septemba 10, 2023, wachimbaji wawili walipoteza maisha na wengine 28 kuokolewa baada ya kuingia kwenye eneo lililofungwa la mgodi wa Kanegere, Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita na kuporomokewa.
Lingine lililopoteza maisha ya wengi ni tukio la Juni 20, 2022, katika mgodi wa Mirelani mkoani Arusha, wachimbaji 42 walifariki dunia baada ya pampu ya oksijeni kushindwa kufanya kazi. Ajali hiyo ilisababisha Serikali kusitisha shughuli zote za uchimbaji kaskazini mwa nchi kwa muda.
Mgodi wa Nyangarata mkoani Shinyanga Oktoba 5, 2015, uliporomoka na kusababisha kifo cha mchimbaji mmoja, huku wengine 41 wakinusurika baada ya kukaa kwa siku 41 chini ya ardhi.