Maombi ya zaidi ya nchi 50 za dunia ya kuwekewa vikwazo vya silaha utawala wa Kizayuni

Kufuatia kuendelea mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na Lebanon, zaidi ya nchi 50 za dunia zimemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na Baraza Kuu la umoja huo wauwekee vikwazo vya silaha utawala huo katili.

Miezi 13 imepita tangu kuanza mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo pandikizi dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Katika kipindi hiki, zaidi ya Wapalestina 43,000 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 100,000 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake. Mbali na hujuma za kila siku, utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu umepelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya watu huko Gaza kutokana na siasa zake za kikatili za kusababisha njaa kali na kuzuia kutumwa misaada ya kibinadamu hususan chakula na dawa kwa wakazi wa Gaza. Uhalifu huo wa kivita pia unatekelezwa dhidi ya watu wa Lebanon tangu miezi miwili iliyopita.

Mateso na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina

Nchi za Magharibi hususan Marekani kwa kuutumia utawala haramu wa Israel kila aina ya misaada ya wazi na ya siri ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi zinashirikiana wazi na utawala huo katika kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon. Kuna ushahidi mkubwa na wa kutosha kuwa silaha zinazotumwa na nchi hizo kwa utawala wa Kizayuni zinatumika katika vitendo vya kikatili vinavyofanywa na utawala huo dhidi ya raia wa Palestina na Lebanon. Huu ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Mfano wa wazi kuhusu suala hilo ni utumiaji wa mabomu ya tani moja ya kuvunja miamba yaliyotengenezwa Marekani katika mauaji ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah ya nchini Lebanon.

Awali, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha marufuku ya kutuma silaha katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel baada ya nchi 28 kupiga kura ya kuunga mkono marufuku hiyo. Pia, nchi 6 zilipiga kura ya kupinga marufuku hiyo na 13 hazikupiga kura kabisa. Marekani na Ujerumani ni miongoni mwa nchi hizo chache zilizopiga kura kupinga marufuku hiyo. Nchi hizi 2 ndio wasambazaji wakubwa wa silaha kwa utawala wa Kizayuni. Marekani hutuma silaha nyingi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) kuliko nchi nyingine yoyote. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Washington imetoa zaidi ya dola bilioni 17 za misaada ya kijeshi na kiuchumi kwa utawala huo haramu. Baada ya Marekani, Ujerumani na Italia ndizo nchi zinazopeleka silaha kwa wingi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.

 Sayyid Hassan Nasrullah; Shahidi wa Njia ya Quds na Palestina

Kwa kuendelea mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon na katika hali ambayo jamii ya kimataifa imeshindwa kabisa kusimamisha jinai hizo za kinyama, zaidi ya nchi 50 zimetaka kuchukuliwa hatua za dharura kwa ajili ya kusimamisha kupelekwa silaha katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo katili. Zaidi ya nchi 50 zimeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu kuchukua hatua madhubuti na za haraka ili kuzuia kuuziwa au kupewa silaha utawala huo. Ombi hilo limetolewa huku idadi ya wahanga wa vita katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi ikiongezeka kwa kasi.

Kuhusu suala hilo tunaweza kusema kuwa ombi la nchi hizo 50 mbali na kuthibitisha ushiriki wa nchi zinazouza silaha katika mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na vile vile huko Lebanon, pia linaonesha kuwa, nchi hizo za Magharibi zinahusika moja kwa moja katika kuchochea ghasia dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon na wakati huo huo kuzuia mfumo wa kimataifa kutekeleza majukumu yake ya kisheria dhidi ya utawala huo unaotenda jinai za kutisha ulimwengu bila kuogopa lolote.