
Baada ya ligi ya kikapu ya daraja la kwanza kumalizika, takwimu zimeonyesha hakuna mchezaji yeyote aliyepewa adhabu ya kumchezea makosa mwenzake ya siyo ya kimchezo (unsportsman).
Makosa yasiyo ya kimchezo ni yale mchezaji anayemshika jezi mwenzake au kumzuia kwa mguu.
Kamishina wa Makocha wa Shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF), Robert Manyerere, amesema endapo mchezaji atafanya kosa hilo, mwamuzi atatoa adhabu ya mitupo huru miwili kuelekea upande kwa yule aliyefanya makosa hayo.
Alisema kabla ya hapo mwamuzi atapiga filimbi ya kuashiria kosa hilo, kwa kunyoosha ngumi moja juu na mkono mwingine ukishika mkono huo.
Naye Kamishina wa ufundi wa chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD), Haleluya Kavalambi amesema wachezaji wa timu zilizoshiriki Ligi hiyo walifuata sheria za uchezaji.
“Ndiyo maana matukio ya kiajabu, ajabu yanayofanywa na wachezaji, katika Ligi hii hayakutokea,” alisema Kavalambi.
Timu zilizoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza mkoa wa Dar es Salaam, ni Polisi, Stein Warriors, Kurasini Heat, Chang’ombe Boys, Mlimani B.C, Mbezi Beach, Kingamboni Heroes, Yellow Jacket na Kibada Riders.
Nyingine ni PTW, Christ the King, Magone, Premier Academy, Dar Kings, Donbosco VTC, Mgulani Warriors, Magnet na St. Joseph.