
Kocha Mkuu wa Tabora United, Genesis Mang’ombe amesema hatakubali kuwa mnyonge na kuruhusu kikosi chake kucheza mchezo wa nne bila kupata ushindi huku akitaja mambo yaliyowaangusha kwenye mechi zilizopita.
Mang’ombe raia wa Zimbabwe ambaye amerithi mikoba ya Mkongomani, Anicet Kiazmak aliyeiongoza Tabora United katika mechi 14 na kushinda nane, sare tano na kupoteza moja, tayari ameshapoteza mechi tatu.
Tangu kuondoka kwa Kiazmak, timu hiyo imecheza mechi nne (mbili za Ligi Kuu na mbili za Shirikisho) na kushinda moja pekee dhidi ya Transit Camp (penalti 4-2), huku ikifungwa na Yanga (3-0), JKT Tanzania (2-1) na Kagera Sugar (penalti 5-4) kwenye Shirikisho.
Tabora United kesho Jumamosi Aprili 4, 2025 itakuwa ugenini katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kucheza mchezo wa raundi ya 25 dhidi ya Pamba Jiji utakaopigwa kuanzia saa 8:00 mchana.
Akizungumzia maandalizi ya timu yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Ijumaa jijini Mwanza, Mang’ombe amesema licha ya kupoteza mbele ya Yanga lakini wamefanya maandalizi mazuri na watafanya mabadiliko ya wachezaji na kupumzisha wengine ili kupata nguvu mpya kwenye timu.
Amesema wamefanyia kazi baadhi ya vitu vilivyowaangusha kwenye mechi zilizopita ikiwemo udhaifu katika kushindania mipira dhidi ya wapinzani wao na kuruhusu mabao mepesi ambayo timu ya hadhi yake haipaswi kufungwa.
“Mchezo wa soka siku zote tunayapokea matokeo yanayokuja kisha unarudi kwenye ubaoni kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza, kila mmoja anaelewa kwa nini tunapoteza mechi tunaruhusu mabao yaleyale ambayo hayavumiliki kwa kiwango tulichopo sisi,” amesema Mang’ombe.
Ameongeza kuwa, “nimekuwa nikilifanyia kazi hilo hii ni ligi ya kiushindani na hatutegemei kufungwa magoli ya aina ile, na hata ukiangalia mechi iliyopita wenzetu walikuwa na nguvu kubwa kuliko sisi na walituzidi.”
“Na hilo ni jambo lingine ambalo tumekuwa tukilifanyia kazi kujituma, kushindana haswa na kuishinda mipira dhidi ya mpinzani na nafikiri mwisho wa siku tutapata matokeo mazuri.”
Mzimbabwe huyo amelia na ufinyu wa ratiba ambao unamnyima nafasi ya kufanya maandalizi ya kutosha kwani walicheza na Yanga Aprili 2, 2025 mjini Tabora na kesho Aprili 5, watacheza jijini Mwanza dhidi ya Yanga.
“Tunao wachezaji wa kutosha na inabidi tupumzishe wengine na kuwatumia wapya kuleta nguvu mpya, nina muda mfupi kwenye timu kwahiyo kufanya mabadiliko ya kikosi inaweza kuwa ngumu pia kwetu ni mtihani mkubwa ukiangalia hatujapata muda wa kutosha wa kupumzika,” amesema Mang’ombe.
Amesema: “Lakini tunapaswa kufuata ratiba iliyopangwa na mwisho wa siku tunataka alama hivyo tunahitaji kuhamasisha wachezaji kujitoa kwa uwezo wao ili tuondoke na ushindi.”
Mchezaji wa timu hiyo, Rajab Masinga amesema: “Licha ya kupoteza dhidi ya Yanga lakini saikolojia yetu imerudi palepale mpango haukuwa ni kucheza mechi tu dhidi ya Yanga bali kucheza mechi zote zilizo mbele yetu ili tuhakikishe msimu huu tunamaliza ligi katika nafasi nzuri.”