
Mwenendo wa maisha ya wazazi unajumuisha maneno, matendo, tabia, mila, na desturi wanazozitumia kuendesha maisha yao ya kila siku.
Mwanafalsafa Shadrack Gamaldhin kutoka Gambia aliwahi kusema: “Maneno yako ndiyo matendo yako, matendo yako ndiyo tabia yako, tabia yako ndiyo desturi yako na desturi yako ndiyo maisha yako.”
Kauli hii inatoa msingi wa kuelewa jinsi malezi yanavyoathiri maisha ya watoto.
Tunapotafakari maneno haya kwa undani, tunabaini kwamba tabia na desturi za wazazi ni picha halisi ya mwenendo wa maisha yao, ambayo inaonekana machoni mwa watoto wao. Gamaldhin anazungumzia uwezo wa ubongo wa mwanadamu kupokea na kuhifadhi kumbukumbu tangu utotoni.
Wataalamu wa makuzi wanasema mtoto mdogo ana uwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa, ambazo baadaye hutumika kutatua changamoto katika maisha.
Kwa maana hiyo, tafiti nyingi zinasisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto wao.
Hata hivyo, katika nyakati za sasa, kumekuwa na changamoto nyingi za maadili, na kila mzazi ana njia yake ya kulea watoto.
Wakati wazazi wengine hawafuati njia inayopaswa, ukweli unabaki kuwa wazazi wanapaswa kujiheshimu na kutenda matendo mema mbele ya watoto wao.
Mazungumzo yanayofanywa mbele ya watoto ni muhimu sana. Watoto hawazaliwi wakiwa na msamiati wa matusi; wanajifunza kutoka kwa wazazi na jamii inayowazunguka.
Tabia na misemo ya kila siku huunda mtazamo wa mtoto kuhusu maisha, lugha, na uhusiano. Wengi hudhani kuwa malezi bora yanahusu kumpatia mtoto mahitaji ya kimsingi tu, lakini kwa hakika mzazi anapaswa kumjengea misingi imara ya maisha.
Methali ya Kiswahili isemayo “Kuzaa si kazi, kazi ni kulea” inaakisi ukweli huu. Wazazi wanapaswa kuwa mfano bora kwa watoto wao, kwani urithi mkubwa anaoupata mtoto kutoka kwao ni namna ya kuishi na watu wengine.
Pia kuna tatizo linalozidi kukua la mawasiliano hafifu kati ya wazazi, ambapo wanakaripiana au kutukanana mbele ya watoto.
Hali hii huathiri mtazamo wa watoto kuhusu uhusiano wa kifamilia. Kama wazazi wanazozana mara kwa mara mbele ya watoto, hawa watoto huchukua tabia hizo kama sehemu ya maisha ya kawaida.
Matokeo yake ni kwamba watoto hao huweza kukumbwa na changamoto za kimaadili na kijamii wanapokuwa wakubwa.
Wazazi wanapaswa kuwa makini katika matendo na maneno yao mbele ya watoto. Kila kitendo wanachofanya kina athari kubwa katika kujenga tabia na maisha ya baadaye ya watoto wao. Malezi bora si tu kuwapa watoto chakula na mavazi, bali pia kuwaongoza kwa mfano bora wa tabia na maadili.
Mzazi anatunza maadili kwa kutumia njia mbalimbali zinazosaidia kumjengea mtoto msingi imara wa tabia njema na maadili mema. Njia hizi zinajumuisha:
Kwa mfano, watoto hujifunza zaidi kwa kuiga, hivyo ni muhimu kwa mzazi kuonyesha matendo na tabia ambazo wanataka watoto wao waige. Hii inamaanisha kuwa na mwenendo mzuri, kuheshimu wengine, kusema ukweli, na kutenda haki. Mtoto anapoona mzazi wake akiishi kwa maadili, naye atafuata mfano huo.
Mzazi anapaswa pia kumfundisha mtoto maadili ya kijamii kama vile heshima, uvumilivu, ushirikiano, na upendo.
Hii inaweza kufanywa kupitia mazungumzo ya kila siku, hadithi, au kushirikiana katika shughuli za kijamii zinazofundisha maadili haya.
Lakini pia si vibaya kama ataweka sheria za familia na kuhakikisha zinazingatiwa, ni njia ya kumfundisha mtoto kuhusu matendo mema na mabaya.
Nidhamu inaonyesha mtoto kuwa kila tendo lina matokeo na hivyo inamsaidia kuendeleza uwajibikaji na kujizuia kufanya makosa.
Kuna mazungumzo yenye lengo la kufundisha na kuelekeza, haya yana nafasi kubwa katika kutunza maadili.
Mzazi anapaswa kutumia muda kuzungumza na mtoto kuhusu maadili mema, umuhimu wa kuwa na tabia nzuri, na jinsi ya kufanya maamuzi sahihi katika maisha.
Nawaza kwa sauti kuu kwamba, kwa kutekeleza mambo haya machache niliyoyaainisha, mzazi anaweza kuimarisha maadili na tabia njema kwa watoto wake na kuwaandaa kwa maisha bora ya baadaye.