Maneno ‘mwanamume suruali’ yalivyosababisha mauaji kituo cha Polisi

Musoma. Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa, mkazi wa kijiji cha Mkengwa katika wilaya ya Tarime, Wangoko Matienyi, kwa kosa la kumuua mgambo kwa kumchoma kisu mbele ya mlango wa kituo cha Polisi.

Mauaji hayo yalitokea Agosti 30,2022 kituo cha Polisi cha Kibuyi, wakati marehemu, Fred Obunga akimzuia Matienyi asimfikie mkewe aliyekimbilia kituoni hapo, baada ya mumewe huyo kumkimbiza akiwa ameshika kisu kwa lengo la kumuua.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliieleza mahakama kuwa mkewe huyo alikuwa amemtolea maneno ya kuudhi kwa kumtamkia kuwa yeye ni ‘mwanamume suruali’,  maneno yaliyomfanya amkimbize hadi kituo cha Polisi.

Hukumu hiyo imetolewa jana Jumatatu Machi 10, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Fahamu Mtulya, ambaye alisema anaamini upande wa mashitaka umethibitisha shitaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha mashaka.

“Mahakama imethibitisha mshtakiwa alimuua marehemu akiwa na dhamira ovu ya kufanya mauaji. Ninashawishika kuamini kuwa Jamhuri wamejenga kesi yao kulingana na kifungu cha 3(2)(a) cha sheria ya ushahidi,” alisema Jaji Mtulya.

“Katika kesi hii, mshtakiwa hakubisha kuwa alimuua marehemu Agosti 30, 2022 na hakubisha kupokelewa kwa taarifa ya uchunguzi wa kifo na kumbukumbu za mahakama zinaonyesha aliomba kukiri kosa dogo la kuua bila kukusudia,” alisema.

Jaji alisema tangu wakati wa kusomewa kosa lake, hatua ya usikilizwaji wa awali na wakati wa usikilizaji wa kesi alikuwa akiomba kukiri kosa la kuua bila kukusudia, lakini kwa ushahidi uliopo alikuwa na dhamira ovu.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji alisema mshtakiwa alifikishwa kortini kwa mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu 196 na 197 cha Kanuni ya adhabu na Mahakama imemtia hatiani kwa kosa hilo ambalo adhabu yake ni kifo.

Mke alivyomkaanga mumewe

Shahidi wa Ppli wa Jamhuri, Nyasurati Chacha, alieleza kiini cha mzozo baina yake na mumewe hadi kuamua kukimbilia kituo cha polisi kwa sababu ya usalama wake na mauaji yalivyotokea kituoni hapo akiyashuhudia.

Shahidi huyo alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 30, 2022 mchana wakati mshtakiwa akimfukuza kwa dhamira ya kumshambulia kwa kisu kama mfululizo wa matukio ya visa na mikasa yaliyoanzia Agosti 29,2022.

Akichambua ushahidi huo, jaji alisema shahidi huyo alieleza kuwa mshtakiwa alikuwa akitoa maneno ya vitisho dhidi yake wakiwa nyumbani na kituo cha polisi akimtuhumu kuwa ni malaya jambo ambalo halikuwa kweli.

Kutokana na maneno ya vitisho, aliamua kumtoroka mshtakiwa na kukimbilia kituo cha Polisi, mshtakiwa alimfuatilia kwa kumkimbiza, lakini walipofika kituoni, mshtakiwa alizuiwa na marehemu katika ngazi za mlango wa kuingia kituoni.

Alieleza alishuhudia mshtakiwa (mumewe) akimshambulia marehemu kwenye mkono na kwenye shingo kwa kutumia kisu alichokuwa amekishika.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, mshtakiwa alikuwa analazimisha kuingia kwa nguvu kituo cha Polisi cha Kibuyi ambapo alizuiwa mlangoni na marehemu.

Kulingana na shahidi huyo, baada ya mshtakiwa kuzuiwa na marehemu, aliamua kumng’ata mkono na baadaye kumshambulia kwa kisu shingoni upande wa kushoto na kufanikiwa kutoroka kutoka katika eneo la tukio bila kukamatwa.

Ushahidi wa mashahidi wengine

Simulizi ya shahidi huyo wa pili, iliungana na ushahidi wa shahidi wa tatu, Koplo Tumaini Ruhaga ambaye alikuwepo kituoni hapo wakati tukio hilo la mauaji likitokea. Alishuhudia mauaji hayo mabaya kituoni.

Shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo ya tukio, alishuhudia mshtakiwa akiwa na kisu akimfukuza shahidi wa pili (mkewe) na alizuiwa na marehemu katika ngazi za kuingia mlango wa kituo cha Polisi ambaye alimtaka akae nje ya kituo.

Badala ya kukaa nje kama alivyoamriwa, mshtakiwa alikuwa analazimisha kuingia kwa nguvu kituoni ili kumfuata mpenzi wake, hapo ndipo kulipotokea ugomvi baina ya mshtakiwa na marehemu akiwa analazimisha kuingia kituoni.

Ni katika tafrani hiyo, mshtakiwa alimng’ata marehemu kwenye mkono na kumshambulia kwa kisu mapigo mawili shingoni na kusababisha kifo  na walishindwa kumkamata kutokana na kuwa na kisu.

Kulingana na shahidi huyo, baada ya kumshambulia marehemu kwa kisu na kupoteza maisha, mshtakiwa aliendelea kutoa vitisho kuwa angemuua mtu yeyote ambaye angemsogelea na ni katika mazingira hayo alifanikiwa kutoroka.

Shahidi wa nne wa Jamhuri ambaye hata hivyo hukumu hiyo haikumtaja jina, alieleza kuwa siku ya tukio alishuhudia mshtakiwa akimfukuza shahidi wa pili wa Jamhuri ili kumshambulia, na shahidi huyo alikuwa amekimbilia kituoni.

Hapo kituoni, mshtakiwa alizuiwa kwenye ngazi za kuingia mlango wa kituo cha Polisi na marehemu na akawa anakataa kuzuiwa huko ndipo akaanza kupigana na marehemu, ambapo alimng’ata na kumchoma kisu.

Shahidi wa sita, koplo Saidi ambaye alikuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alielezea namna alivyopeleleza na baadaye kufanikiwa kumkamata mshtakiwa, huku daktari akisema visu vile vilipasua mishipa ya damu.

Utetezi wa mshtakiwa

Katika utetezi wake, mshtakiwa akiri maelezo yaliyotolewa kuwa Agosti 30,2022 alikuwa akimfukuza mkewe kutoka eneo lake la kazi (la mume) hadi kituo cha Polisi cha Kibuyu baada ya kumtakia maneno mabaya ‘mwanamme suruali’.

Kulingana na mshtakiwa, siku hiyo alikuwa ameitwa na bosi wake aitwaye Mabutu Egina Ndara anayejishughulisha na uvuvi ili kutengeneza kamba na nyavu na wakati anaendelea na kazi alitokea shahidi wa pili ambaye ni mkewe.

Aliendelea kueleza kuwa mkewe alianza kumtolea maneno ya kudhalilisha na ndipo akaamua kumfuata bila kujua (mshtakiwa) ana kisu mfuko wa nyuma na walipofika kituo cha Polisi alimkuta mgambo aitwaye Kimogo.

Mgambo huyo alikuwa na ofisa mmoja wa Polisi kituoni hapo, ambapo mgambo huyo alimsihi kupunguza hasira na kutii amri iliyomtaka kukaa jirani na kituo.

Hata hivyo, alieleza kuwa marehemu aliacha eneo lake la kazi kituo cha Polisi na ghafla akamfuata na kuanza kumzaba vibao mgongoni na baadaye alimpiga miguuni kwa kutumia rungu, hivyo alishindwa kuvumilia kipigo hicho.

Hivyo aliamua kujilinda kwa kujibu mapigo kwa kumshambulia marehemu mara moja kwa kisu na hakumbuki ni eneo gani la mwili alimpiga wakati wakipigana na alitoroka kwa hofu, kwani ni tukio lake la kwanza.

Mwisho wa utetezi wake kwa mujibu wa jaji, mshtakiwa aliiomba Mahakama ikubali ahukumiwe kwa kosa la kuua bila kukusudia akidai kuwa alimuua marehemu bila nia yoyote ovu wala dhamira mbaya, bali ilichangiwa na ugomvi na mkewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *