
Manchester United inapambana kuhakikisha straika wa Napoli na Nigeria, Victor Osimhen anayecheza kwa mkopo Galatasaray anatua katika kikosi chao msimu ujao, lakini changamoto inayoweka dili hilo matatani inaonekana ni hitaji la mshahara pamoja na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Hadi sasa Man United ina asilimia chache kucheza Ligi ya Mabingwa kupitia nafasi nne za juu na njia pekee inayoonekana huenda ikaiwezesha kufanikisha hilo ni kupitia Europa League.
Osimhen alikuwa karibu kutua England dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini ilishindikana baada ya Chelsea kushindwa kumpa ofa ya mshahara aliohitaji. Man United imeamua kujitosa tena.
KIUNGO wa Manchester United na Brazil, Casemiro, 32, amewaambia mabosi kwamba anahitaji kupewa mshahara wake wote wa miezi 16 uliobaki ikiwa wanataka aondooke dirisha lijalo. Casemiro ambaye mshahara wake kwa wiki ni Pauni 300,000 awali alihusishwa na dili la Saudi Arabia lakini inadaiwa amegoma hadi Man United itakapompa pesa hizo na ikishindikana ataendelea kusalia hadi mwisho wa msimu ujao.
MANCHESTER City imeongeza juhudi katika harakati za kutaka kumsajili kiungo wa Bayer Leverkusen na Ujerumani, Florian Wirtz, ikiwa ni katika mipango ya kujiandaa na maisha bila ya Kevin de Bruyne anayeweza kuondoka Etihad mwisho wa msimu huu. Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, Leverkusen inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 85 milioni ili kumuuza Wirtz.
MANCHESTER City imepokea ofa kibao kutoka timu mbalimbali za Saudi Arabia, Ureno na Hispania zinazotaka saini ya kiungo raia wa Ureno, Bernardo Silva katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Tangu dirisha kubwa mwaka jana, Silva amekuwa akiwindwa na matajiri wa Saudi Arabia waliodaiwa kumpa ofa ya zaidi ya Pauni 400,000 kwa wiki, lakini alikataa.
BORUSSIA Dortmund inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 85 milioni ili kumuuza winga raia wa England, Jamie Gittens, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi barani Ulaya. Huduma ya mchezaji huyo anayeichezea timu ya taifa ya vijana ya England chini ya umri wa miaka 22 imekuwa ikimezewa mate na Arsenal, Tottenham Hotspur na Chelsea.
BEKI wa Bournemouth na Hispania, Dean Huijsen, 19, ana kipengele kinachomruhusu kuondoka kwa Pauni 50 milioni katika klabu hiyo kuanzia dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya. Mchezaji huyo anayewindwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu England, hususani Liverpool amekuwa katika kiwango bora kabisa msimu huu jambo lililozivutia timu nyingi kutaka kumsajili mwisho wa msimu.
MANCHESTER United inatarajia kukunja Pauni 31 milioni kupitia dili la straika wa Marseille, Mason Greenwood, 23, kwenda PSG dirisha la kiangazi. Katika makubaliano ya mauzino Man U na Marseille kulikuwa na kipengele Man United itapata asilimia 50 ya ada ya uhamisho staa huyo atauzwa. PSG imeweka mezani Pauni 62 milioni ikimtaka.
BAYERN Munich imeachana na mpango wa kutaka kumsajili beki wa Bayer Leverkusen, Jonathan Tah, 29, ambaye ameonyesha uhitaji wa kutua Barcelona zaidi katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Tah ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu aliweka wazi hataongeza na ataondoka kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya.