
Inaelezwa kwamba Manchester City imefikia hatua nzuri katika harakati za kuiwania saini ya winga wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Ujerumani, Florian Wirtz kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyu huduma yake inahitajika na timu nyingi ikiwamo Real Madrid na Bayern Munich lakini, matajiri hao wa Jiji la Manchester City wameshafikia hatua nzuri katika mazungumzo na mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kujiunga nao.
Timu nyingi zilianza kuvutiwa na Wirtz baada ya kiwango bora alichoonyesha msimu uliopita katika michuano ya Bundesliga na Europa League lakini zilishindwa kumsajili katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na badala yake akaendelea kusalia Leverkusen.
Tangu kuanza kwa msimu huu Wirtz amecheza mechi 39 za michuano yote, amefunga mabao 15 na kutoa asisti 13.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027 na Leverkusen inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza mchezaji huyu.
Mile Svilar
Chelsea na Manchester City ni kati ya timu zinazohitaji saini ya kipa wa AS Roma na timu ya taifa ya Serbia, Mile Svilar, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Svilar amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa timu hizi kwa muda sasa na anaonekana kuwa mtu sahihi kwao kutokana na mahitaji yao kwa msimu ujao. Mkataba wa kipa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Lamare Bogarde
SEVILLA inajipanga kutuma ofa kwenda Aston Villa ili kuipata huduma ya kiungo wa timu hiyo mwenye umri wa miaka 21, Lamare Bogarde, mwisho wa msimu huu.
Bogarde pia ameonyesha nia ya kuwa tayari kuondoka ili kupata nafasi kubwa zaidi ya kucheza tofauti na ilivyo sasa.
Msimu huu amecheza mechi 18 za michuano yote.
Johan Martinez
Manchester City, Bayer Leverkusen, Parma na Wolfsburg zimeendelea kupigana vikumbo katika kuiwania saini ya kiungo wa Independiente del Valle raia wa Ecuador, Johan Martinez, 15, kuelekea dirisha lijalo.
Maskauti wa timu hizi wanadaiwa kutembelea Ecuador kwa ajili ya kumtazama Martinez ambaye ni mmoja kati ya wachezaji makinda wenye viwango vikubwa.
Antonio Cordero
NEWCASTLE United inapewa nafasi kubwa ya kuzipiku Real Madrid na Barcelona katika dili la kuiwania saini ya mshambuliaji wa Malaga na Hispania, Antonio Cordero, 18, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Cordero amepanga kujiunga Newcastle badala ya Barca na Madrid kwa sababu anaamini atapata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kalvin Phillips
KIUNGO wa Manchester City, Kalvin Phillips, 29, amewaambia wawakilishi wake kwamba yupo tayari kurudi Leeds United katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa timu hiyo itapanda tena Ligi Kuu.
Phillips ambaye msimu huu anacheza kwa mkopo Ipswich Town, mkataba wake na Man City unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Benjamin Cremaschi
TOTTENHAM inadaiwa kuwasilisha ofa kwenda Inter Miami kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo, Benjamin Cremaschi, 20, katika dirisha lijalo.
Licha ya kuhitajika na timu nyingi za England, staa huyu wa kimataifa wa Marekani, sio mmoja kati ya mastaa wanaopata nafasi kubwa ya kucheza kwenye kikosi cha Miami na msimu huu amecheza mechi 8 za michuano yote. Mkataba wake unamalizika mwaka 2027.
Semih Kilicsoy
NEWCASTLE United inaongoza katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Besiktas, Semih Kilicsoy, 19, kuelekea dirisha lijalo.
Fundi huyu ambaye pia anahitajika na Aston Villa, Fulham, Everton na Nottingham Forest, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.