Man United yajiweka pazuri Europa

Manchester, England. Bao la dakika za mwisho lililofungwa na kiungo wa Manchester United Bruno Fernandes, limetosha kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Rangers kwenye mchezo wa Europa.

Ushindi huo umeifanya United kuwa na uhakika wa kufuzu moja kwa moja kwenye hatua ya mtoano ya michuano hiyo.

Awali United ilifanikiwa kufunga bao la kwanza kutokana na makosa ya kipa wa Rangers raia wa England Jack Butland, kuokoa mpira kizembe na kuupeleka wavuni katika dakika ya 52.

Rangers ikiwa inaonyesha kiwango cha juu ilifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa  Cyriel Dessers dakika ya 88, kabla Bruno hajafunga la pili dakika mbili za nyongeza.

Awali kabla ya mabao hayo, United ilifunga kupitia kwa Matthijs de Ligt lakini likakataliwa kutokana na beki Leny Yoro kufanya madhambi kabla bao hilo halijafungwa.

United tofauti na inavyofanya kwenye ligi kuu, huku imeonekana kuwa bora kutokana na kushinda michezo minne kati ya saba iliyocheza, ikiwa haijapoteza wowote.

Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 15 zikiwa ni nne tu nyuma ya vinara wa kundi Lazio wenye pointi 19 kileleni, timu inayoshika nafasi ya pili ni Eintracht Frankfurt ambayo imekusanya pointi 16 ikiwa sawa na Athletic Club, hii inaonyesha kuwa United baada ya mchezo wa mwisho itakuwa na nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano moja kwa moja.

Baadhi ya matokeo mengine ya Europa, Poak waliichapa Slavia Praha mabao 2-0,  Entracht waliifunga Ferancvaros mabao 2-0, Ajax ilishinda 1-0 dhidi ya RFS huku Nice ikilala 1-0 dhidi ya Elfsborg.