Man United yabeba kinda mwingine Arsenal

London. Manchester United leo Februari 2, 2025 imekamilisha usajili wa beki wa kati Ayden Heaven kwa mkataba wa miaka minne na nusu.

Mchezaji huyo amenaswa kwa dau la fidia kwa Arsenal ambalo halijawekwa wazi na klabu zote mbili.

Kinda huyo aliyeitumikia Arsenal akichezea vikosi vya vijana kwa miaka mitano, amesema kuwa amefurahia kujiunga na Manchester United.

“Ninaona fahari kubwa kujiunga na Manchester United. Ninamshukuru kila mmoja aliyesaidia ndoto hii kuwa uhalisia.

“Kuna mengi ambayo nataka kuyapata katika mchezo. Nitatoa kila nilichonacho kuendeleza maendeleo yangu na kuwa mchezaji bora ninavyoweza kuwa,” amesema Heaven.

Mkurugenzi wa ufundi wa Manchester United, Jason Wilcox amesema kuwa beki huyo atapelekwa moja kwa moja katika kikosi cha wakubwa

“Klabu hii ina rekodi ya aina yake ya kusapoti wachezaji wadogo na tunaamini Heaven yupo katika mahali sahihi kufikia matarajio makubwa ya ubora wake.

“Tuna furaha kwamba Ayden amejiunga na Manchester United.  Tayari ni beki mwenye kipaji ambaye yuko tayari kujiunga na kikosi chetu cha kwanza ili kupata maendeleo yake,” amesema Wilcox.

Heaven anakuwa mchezaji wa pili wa Arsenal kujiunga na Man United msimu huu akifuata nyayo za mshambuliaji Chido Obi-Martin (17) aliyesajiliwa mwezi Oktoba mwaka jana.

Katika dirisha hili dogo la usajili, Manchester United imemsajili pia beki wa kushoto, Patrick Dorgu kutoka Lecce ya Italia.