Manchester United na Tottenham zimejikuta zikikosa ushindi katika michezo yao ya kwanza kwenye mashindano ya Ligi ya Europa iliyochezwa jana.
Katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Anoeta ambao unamilikiwa na Real Sociedad, Man United ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Joshua Zirkzee katika dakika ya 57 ambapo alimalizia pasi ya Alejandro Garnacho.
Dakika ya 70 Mikel Oyarzabal aliifungia Real Sociedad bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti baada ya nahodha wa United, Bruno Fernandez kushika mpira kwenye eneo la hatari na mechi hiyo kumalizika kwa sare.

Baada ya mchezo huo kumalizika, United itacheza mchezo wa marudiano wiki ijayo kwenye Dimba la Old Trafford huku ikihitaji matokeo ya ushindi kusonga katika hatua ya robo fainali.
Mara ya mwisho United kufanya vizuri kwenye mashindano haya ilikuwa ni mwaka 2017 ilipotwaa ubingwa kwa kuifunga Ajax mabao 2-0.
Wakati United ikibanwa kwa sare, Tottenham yenyewe ilikubali kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya AZ Alkmaar katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa AFAS.
Tottenham ilijifunga bao katika dakika ya 18 kupitia kwa Lucas Bergvall ambaye alikuwa kwenye harakati za kutaka kuzuia mpira uliopigwa langoni kwao.
Tottenham italazimika kutafuta ushindi katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Machi 23, 2025 kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspur, London.
Katika michezo mingine iliochezwa jana ulitia gumzo zaidi ni ule wa Fenerbahçe dhidi ya Rangers.

Katika mchezo huo ambao Fenerbahçe ilifungwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani kocha mwenye maneno mengi Jose Mourinho alionekana kuchanganyikiwa na kipigo hicho jambo lililomfanya aonekane kama amelala wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi kumalizika.
Matokeo ya mechi nyingine zilizochezwa jana
FCSB 1-3 Lyon
Ajax 1-2 Eintracht Frankfurt
Bodø/Glimt 3-0 Olympiacos
Roma 2-1 Athletic Club
Viktoria Plzeň 1-2 Lazio