Man United sasa mambo magumu zaidi

Manchester, England. Maisha ya Manchester United yanaendelea kuwa mabaya kila kukicha jambo ambalo linaonyesha kuwa maisha ya makocha kwenye timu hiyo yatazidi kuwa mabaya kila msimu.

Jana United iliendelea kuwa kwenye wakati mbaya katika Ligi Kuu England baada ya kulala kwa mabao 3-1 dhidi ya Brighton mchezo uliopigwa Uwanja wa Old Trafford na kuendelea kuporomoka kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo mpaka sasa timu zimeshacheza michezo 22.

Hii ina maana kuwa kwa sasa United imepoteza michezo sita kati ya 12 iliyocheza kwenye Uwanja Old Trafford, ikiwa ni rekodi mbaya zaidi kwa kikosi hicho kwa kipindi cha miaka 131,  iliyopita yaani ilifanya hivyo tena msimu wa 1893-94, ikiwa inaitwa Newton Heath, na siyo Man United na haikuwa inatumia Uwanja wa  Old Trafford.

Hata hivyo, inaonekana kama siyo msaada wa Amad Diallo ambaye alifunga ‘hat trick’ ya mwishoni kabisa kwenye mchezo mmoja nyuma dhidi ya Southampton, basi United ingekuwa imepoteza michezo saba nyumbani, jambo ambalo ni la kutisha zaidi.

Kwa upande wa Brighton hii ni mechi yao ya tatu wanashinda kwenye ligi dhidi ya United, lakini jambo  la kushtua ni kwamba Brighton wameshinda michezo sita kati ya saba ambayo wamekutana na timu hiyo ya Manchester.

Baada ya mchezo wa juzi, kocha wa United Ruben Amorim, alisema anashtuka kuona timu kubwa kama hiyo inakuwa na kocha mpya lakini inafanya vibaya kuliko wakati ikiwa na kocha aliyepita, jambo ambalo linashtua.

“Hii ni Manchester United mbaya zaidi kwenye historia, ni jambo gumu timu kuwa na kocha mpya lakini inapoteza kuliko hata wakati ikiwa na kocha aliyepita ni mbaya sana na hali hii inaonyesha kuwa bado tuna wakati mgumu kwenye michezo ijayo,” alisema kocha huyo wa zamani wa Spoting Lisbon ya Ureno.

Rekodi ya United inaonyesha kuwa timu hiyo imepoteza michezo sita kati ya nane ya hivi karibuni hali ambayo inazidi kuongeza hofu kwenye kikosi hicho ambacho kinaingia uwanjani Jumapili ijayo kuvaana na Fulham kwenye mchezo mwingine wa ligi hiyo ikiwa nyumbani.

Matokeo ya mchezo huu yanaifanya United kuwa nafasi ya 13 ikiwa na pointi 26, baada ya kucheza michezo 22, kwa sasa timu hiyo ina tofauti ya pointi 10 dhidi ya timu iliyopo kwenye mstari wa kushuka daraja, lakini ikiwa na tofauti ya pointi 24 dhidi ya vinara Liverpool, ikiwa inaonekana kuwa kwenda chini ni rahisi zaidi kuliko kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi.

Mchezo uliopita uliweka rekodi nyingine kwa United baada ya kushindwa kupiga shuti lolote kutokana na shambulizi, jambo ambalo amelijibu kiungo Bruno Fernandez na kusema kuwa ni hali ya mchezo na watarudi kuwa sawa.

“Hili jambo nilikuwa sijalifahamu, lakini tumekuwa tukizungumza kila siku ugumu ambao tumekuwa tukikutana nao kila tunapocheza nyumbani, lakini kwanini timu kubwa kama United ishindwe kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, hili siyo jambo zuri lakini bado tuna nafasi ya kurudi kwenye makali.”

Kwenye michezo 22 ambayo United imecheza kwenye ligi imepoteza kumi, sare tano na kushinda saba, imefanikiwa kufunga mabao 27 tu lakini jambo la kushtua zaidi ni kwamba timu hiyo imeruhusu mabao 32 kwenye michezo hiyo.