Man United mikononi mwa Rangers Europa

Manchester, England. Baada ya kutoka kupoteza mabao 3-1 dhidi ya Brighton, Jumapili Januari 18, 2025 kwenye Ligi Kuu England, Manchester United leo itakuwa na kibarua kingine pale Old Trafford dhidi ya Rangers katika michuano ya Kombe la Europa.

United inashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya matokeo katika Ligi Kuu England ikiwa imetoka kupoteza mechi tatu, sare mechi moja na kushinda mechi moja huku ikiwa imepoteza michezo sita kati ya 12 iliyocheza kwenye Uwanja Old Trafford.

Hii ni rekodi mbaya zaidi kwa kikosi hicho kwa kipindi cha miaka 131,  iliyopita yaani ilifanya hivyo tena msimu wa 1893-94, ikiwa inaitwa Newton Heath, na siyo Man United na haikuwa inatumia Uwanja wa  Old Trafford.

Manchester United inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imekusanya pointi 26 katika michezo 22 huku ikiwa imefunga mabao 27 na kuruhusu mabao 32 katika michezo hiyo.

Kwa upande wa Rangers wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kupata ushindi katika Ligi Kuu ya Scotland ikiwa imeshinda mechi 14, sare mechi tano na kupoteza mechi nne ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 47 katika michezo 23 nyuma ya vinara wa Ligi hiyo Celtic wenye pointi 60.

Licha ya kuonekana kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu England, Manchester United hawajawa wanyonge kwenye michuano ya Ligi ya Europa kwani wamecheza mechi sita bila kupoteza mchezo wowote wakiwa wameshinda mechi tatu na kupata sare  tatu ikishika nafasi ya saba ikiwa na pointi 12.

Wakati United ikiwa nafasi ya saba, wapinzani wao Rangers wenyewe wapo nafasi ya nane wakiwa na pointi 11 katika michezo sita waliocheza ambapo wameshinda mechi tatu, sare mechi mbili na kupoteza mechi moja.

Hali ya msimamo baina ya hizi timu mbili zinaufanya mchezo wa leo kuwa mgumu na wenye ushindani kutokana na kila timu kutafuta ushindi ili kuendelea kubaki katika nane bora.

Wachezaji wanne wa Manchester United, Luke Shaw , Mason Mount , Victor Lindelof na Jonny Evans, bado wapo nje ya uwanja wakiendelea kuuguza majeraha yao.

Marcus Rashford amekosa mechi tisa za mwisho za Manchester United tangu mara ya mwisho alipocheza Europa League dhidi ya Viktoria Plzen Desemba 12, 2024.

Mshambuliaji huyo ataendelea kuwa nje ya kikosi cha Amorim huku kukiwa na sintofahamu juu ya mustakabali wake kwani inaripotiwa huenda akaondoka Klabuni hapo.

Kwa upande wa Rangers, Dujon Sterling, John Souttar, Oscar Cortes, Neraysho Kasanwirjo na aliyewahi kuwa mchezaji wa Manchester United, Tom Lawrence, wote wapo nje kutokana na majeraha. Mohamed Diomande amesimamishwa baada ya kupata kadi tatu za njano katika hatua ya makundi.

Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amekuwa akilalamikia mwendelezo mbaya wa matokeo ambayo kikosi chake kimekuwa kikipata hivi karibuni jambo linalo tishia kibarua chake kwenye viungo hivyo vya Old Trafford.

“Hii ni Manchester United mbaya zaidi kwenye historia, ni jambo gumu timu kuwa na kocha mpya lakini inapoteza kuliko hata wakati ikiwa na kocha aliyepita ni mbaya sana na hali hii inaonyesha kuwa bado tuna wakati mgumu kwenye michezo ijayo,” alisema kocha huyo wa zamani wa Spoting Lisbon ya Ureno.

Amorim ameshinda mechi tano tu kati ya 15 hadi sasa, huku mechi mbili kati ya hizo ameshinda kwenye michezo miwili ya Ligi ya Europa dhidi ya Bodø/Glimt na Viktoria Plzen.

Kwa upande wake kocha wa Rangers, Philippe Clement yeye amesema wanaijua hali wanayopitia Manchester United kwa sasa, lakini wamejipanga kwenda kupambana dhidi yao pale Old Trafford.

“Tunaijua Manchester United ni timu ya aina gani kwa sasa tunafahamu kiwango chao, lakini tunaenda kupambana, na kufanya kitu cha kipekee sana.”

“Timu imefanya kazi kwa bidii sana kufikia nafasi nzuri iliyopo kwa sasa,” alisema Clement