Man U vs Arsenal Mechi ya mawazo tofauti England

Lazima kipigwe. Ndicho unachoweza kusema wakati mashabiki wakisubiri kwa hamu kipute cha Old Trafford, wakati Manchester United itakapoikaribisha Arsenal katika mchakamchaka wa Ligi Kuu England.

Arsenal bado ipo kwenye mbio za ubingwa, hivyo inakwenda Old Trafford kwa jambo moja tu, kushinda mchezo, lakini Man United itacheza mechi ya kulinda heshima yake.

Kwa rekodi za miaka ya karibuni, Arsenal imeifanya Man United kuwa vibonde wao, ambapo katika mechi tano zilizopita, imeshinda nne na kupoteza moja tu, huku ikifunga mabao 10-6. Kwa rekodi hizo, Arsenal ina nafasi kubwa ya kushinda mechi.

Lakini, kwenye rekodi za muda wote kwenye Ligi Kuu England, Man United bado mbabe kwa Arsenal, ambapo katika mechi 65 ilizokutana, imeshinda 26 na kupoteza 21, huku mara 18 ilishinda uwanjani Old Trafford, mahali ambako Arsenal imeshinda tano tu.

Arsenal itashuka uwanjani Old Trafford ikiwa na mzuka wa kutoka kuichapa PSV Eindhoven 7-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Man United iliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Real Sociedad ugenini kwenye Europa League.

Kila timu itakosa wachezaji wake muhimu, ambapo kocha wa Man united, Ruben Amorim hatakuwa na huduma ya Jonny Evans, Mason Mount, Luke Shaw, Lisandro Martinez, Altay Bayindir, Patrick Dorgu, Kobbie Mainoo na Amad Diallo huku wenye hatihati ni Harry Maguire na Manuel Ugarte, wakati upande wa Mikel Arteta kwenye kikosi cha Arsenal, atawakosa Kai Havertz, Gabriel Jesus, Bukayo Saka, Takehiro Tomiyasu na Gabriel Martinelli. Patachimbika.

Mechi nyingine za Jumapili, Chelsea itakuwa mzigoni uwanjani Stamford Bridge kucheza na Leicester City, wakati Tottenham Hotspur nayo itakuwa nyumbani kuikaribisha Bournemouth kwenye moja ya mechi ya kibabe sana.

Leicester City imekuwa na rekodi mbovu msimu huu, itakwenda Stamford Bridge kwa rekodi ya kupoteza mara 19 mbele ya Chelsea katika mechi 35 walizokutana kwenye Ligi Kuu England, huku wao wakishinda sita tu, nne nyumbani na mbili ugenini. Mechi 10 baina yao zilimalizika kwa sare, huku kwenye ushindi wa Chelsea, mara tisa ilikuwa nyumbani na 10 ugenini.

Spurs itakuwa na mechi inayoonekana si ngumu sana kwao kwenye makaratasi kutokana na rekodi zinavyosoma, ambapo kwenye mechi 15 zilizopita, imeshinda 10, sita nyumbani na nne ugenini, huku mechi mbili zilimalizika kwa sare, wakati Bournemouth imeshinda tatu tu, mbili nyumbani na moja ugenini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *