Man City yaambulia tena sare

London. Mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England msimu huu zimezidi kuchangamka baada ya bingwa mtetezi, Manchester City kulazimishwa sare ya bao 1-1 ugenini na Newcastle United.

Ikipewa nafasi kubwa kuibuka na ushindi katika mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa St. James’ Park, Manchester City ilishindwa kulinda bao lake moja ililotangulia kupata katika kipindi cha kwanza na kuwaruhusu wenyeji wao kusawazisha katika dakika za mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Man City ilipata bao lake la kwanza katika dakika ya 35 kupitia kwa Josko Gvardiol aliyemalizia kwa shuti la wastani pasi ya Jack Grealish ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Hilo lilikuwa ni bao la kwanza kwa Gvardiol kuifungia Man City kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu huku akimaliza ukame wa siku 141 alizokaa bila kupachika bao akiwa na timu hiyo tangu alipofunga dhidi ya Fulham, Mei 11, 2024.

Hata hivyo dakika ya 58, Anthony Gordon aliisawazisha Newcastle United kwa mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Jarred Gillett baada ya kipa wa Manchester City, Ederson kumuangusha mfungaji huyo wa bao la Newcastle United kwenye eneo la hatari la Manchester City.

Licha ya kocha wa Man City, Pep Guardiola kufanya mabadiliko ya kuwatoa Ilkay Gundogan, Rico Lewis na Jack Grealish na kuwaingiza Phil Foden, Jeremy Doku na Savinho, timu yake haikuweza kuongeza mabao ambayo yangeipa ushindi.

Ni kama ilivyokuwa kwa Newcastle United ambayo ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Kieran Trippier, Sandro Tonali na Harvey Barnes ambao nafasi zao zilichukuliwa na Joe Willock, Sean Longstaff na Valentino Livramento.

Sare hiyo imeifanya Manchester City kufikisha pointi 14 huku Newcastle United ikifikisha pointi 11.

Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa Manchester City kwenye EPL baada ya wiki iliyopita kulazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Arsenal.