
Manchester, England. Manchester City itatakiwa kufanya kazi ya ziada kama inataka kufuzu kwa hatua ya 16 Bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupangwa kuvaana na Real Madrid kwenye mchezo wa hatua ya mtoano.
Droo ya michuano hiyo imepangwa Nyon Uswis muda mchache uliopita na sasa vigogo hao mmoja itabidi aange mashindano hayo kabla ya hatua ya 16 bora.
Kikosi cha City ambacho kilikuwa hakipewi nafasi kubwa ya kufuzu kwenye hatua ya mtoano kilipata nafasi hiyo kwenye mchezo wa mwisho kabisa baada ya kuichapa Club Brugge mabao 3-1 na kumaliza katika nafasi ya 22.
City imekutana na Madrid mara tatu kwa kipindi cha hivi karibuni na hii itakuwa mara yao ya nne huku timu itakayovuka hapa ikipewa pia nafasi ya kutwaa ubingwa huo msimu huu.
Zilipokutana msimu uliopita, Real Madrid ilifanikiwa kuibuka kidedea baada ya kuichapa City kwenye mchezo wa robo fainali jambo ambalo linawalazimisha City kutumia nguvu kubwa kuhakikisha inaibuka na ushindi wa jumla kwenye michezo hii miwili.
Katika michezo mitano iliyopita ya hivi karibuni Man City imepata ushindi kwenye michezo miwili, huku Madrid nao wakishinda miwili na mchezo mmoja zimetoka sare.
Mechi hizo ambazo kwa sasa zitachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini zitapigwa kati ya Februri 11 na 12 na marudio yatakuwa Februari 18 na 19.
Baada ya City kupangwa na Madrid, vigogo Bayern Munich ambao nao walikuwa kwenye hatihati ya kukutana na wababe hao wamepangwa kuvaana na Celtic.
Mechi nyingine kubwa, PSG itavaana na Brest huku Monaco ambao walionyesha kiwango cha juu msimu huu wakikipiga na Benfica. Kwa upande wa Juventus watacheza na PSV Eindhoven, huku AC Milan wakipangwa na Feyenoord.
Vijana wa Ubelgiji Club Brugge, watakutana na Atalanta ya Italia huku Sporting Lisbon wakivaana na Borussia Dortmund.
Mechi za hatua ya 16 zitapigwa Februari 21 baada ya mechi za Play off kumalizika.
Droo ya jumla:
Real Madridvs Manchester City
Dortmund vs Sporting Lisbon
Atalanta BC vs Club Brugge
AC Milan vs Feyenoord
SL Benfica vs AS Monaco
PSV Eindhoven vs Juventus FC
Bayern Munich vs Celtic FC
Paris Saint Germain vs Stade Brest