
England. Manchester City inaikaribisha Arsenal leo katika Uwanja wa Etihad kuanzia saa 12:30 jioni huku kila moja ikitegemea idara yake iliyo imara zaidi kuwa chachu ya mafanikio katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya England.
Mwenyeji Manchester City matumaini yake makubwa yapo kwa safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa moto wa kuotea mbali kwa kufumania nyavu msimu huu ikitegemea iwe silaha yake dhidi ya Arsenal leo nyumbani kuipatia pointi tatu muhimu.
Katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, safu ya ushambuliaji ya Man City imefunga mabao 11 ikiwa ni wastani wa mabao 2.2 kwa mchezo.
Lakini licha ya kuwa tishio katika kufunga mabao, Man City inaonekana kuwa na udhaifu katika safu yake ya ulinzi kwani katika mechi hizo tano zilizopita, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu ikiwa ni wastani wa bao 0.6.
Inakutana na Arsenal ambayo idara yake imara zaidi ni ya ulinzi ambayo imekuwa hairuhusu mabao kirahisi na kudhihirisha hilo, katika mechi tano zilizopita, imefungwa bao moja tu ikiwa ni wastani wa bao 0.2 kwa mchezo.
Arsenal imeonekana kuwa na udhaifu wa safu yake ya ushambuliaji ambayo imeonekana kuwa butu katika kutumia nafasi na hilo linaweza kuthibitishwa na matokeo ya mechi tano zilizopita za timu hiyo msimu huu ambapo imefunga mabao sita tu ikiwa ni wastani wa bao 1.2.
Hapana shaka ukuta wa Arsenal utakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha tegemeo la Man City katika kufumania nyavu, Erling Haaland hafui dafu leo kama ilivyokuwa katika mechi mbili za msimu uliopita ambao mshambuliaji huyo hakufunga bao dhidi yao kwenye EPL.
Haaland ndiye kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu ya England msimu huu ambapo hadi sasa ameshaweka mpira kimiani mara tisa katika mechi nne zilizopita.
Kana kwamba haitoshi, nyota huyo raia wa Norway amefunga mabao matatu katika mchezo mmoja (hat trick) mara mbili tofauti.
Pointi tatu za kibingwa
Msimu uliopita vita ya kuwania ubingwa wa EPL ilizihusisha timu hizo hadi siku ya mwisho ya kufunga msimu na safari hii zinaonekana kuanza mapema kile kilichotokea katika msimu uliotangulia.
Kabla ya mechi za jana, Manchester City ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 12 huku Arsenal ikiwa ya pili na pointi 10 ambazo imekusanya katika mechi nne ilizocheza hadi sasa za ligi kuu England.
Maana yake timu ambayo itapata ushindi katika mechi ya leo itakuwa imeua ndege wawili kwa jiwe moja ambapo kwanza ni kuvuna pointi tatu na pili kutengeneza pengo la pointi dhidi ya mwenzake.
Ushindi wa Manchester City utaifanya izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na pia itaongeza pengo la pointi kati yake na Arsenal kufikia tano.
Ikiwa Arsenal itapata ushindi maana yake itafanikiwa kuiacha kwenye mataa Manchester City kwa utofauti wa pointi moja.
Majeruhi presha
Arsenal katika mchezo wa leo itawakosa wachezaji watano ambao ni majeruhi huku Man City ikiwakosa wawili na mmoja kuwa hatihati.
Wachezaji watakaokosekana kwa Manchester City ni Nathan Ake na Oscar Bobb huku Kevin De Bruyne akiwa na hatihati huku Arsenal ikiwakosa Martin Odegaard, Oleksandr Zinchenko, Takehiro Tomiyasu, Kieran Tierney na Mikel Merino.
Oliver kuamua kisasi
Manchester City inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na hamu ya kumaliza unyonge wa kutopata ushindi dhidi ya Arsenal katika mechi mbili mfululizo zilizopita za Ligi Kuu England ikitoka sare moja na kufungwa moja.
Arsenal hapana shaka inataka kumaliza kufutwa machozi ya kukosa taji la EPL msimu uliopita kwa tofauti ya pointi mbili na Manchester City ambayo ilitwaa ubingwa.
Kisasi hicho kwa kila timu dhidi ya mwenzake leo kitaamriwa na refa Michael Oliver ambaye ndiye amepangwa kuwa mwamuzi wa kati katika pambano la miamba hiyo.
Man City inaonekana kutokuwa na bahati sana na refa Oliver kulinganisha na Arsenal kwani katika mechi zake tano za hivi karibuni ambazo imechezeshwa na refa huyo, imeshinda tatu, kutoka sare moja wakati Arsenal imepata ushindi mara nne na kupoteza moja.
Oliver atasaidiwa na refa msaidizi namba moja, Stuart Burt na msaidizi namba mbili, Dan Cook huku refa wa nne akipangwa kuwa Andy Madley na katika chumba cha teknolojia ya video kwa waamuzi (VAR) watakuwepo John Brooks na Richard West.
Mechi nyingine ya ligi hiyo leo itakuwa ni baina ya Brighton na Nottingham Forest kuanzia saa 10:00 jioni.
Uhondo wa mahasimu Milan
Jijini Milan, Italia leo kutachezwa mechi ya watani wa jadi wa jiji hilo, Inter Milan dhidi ya AC Milan katika Uwanja wa Giuseppe Meazza kuanzia saa 3:45 usiku.
Timu hizo kubwa kihistoria nchini humo, zinakutana huku kila moja ikiwa haijaanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ na pengine ushindi wa mechi ya leo ukabadilisha upepo kwa timu mojawapo kwa kuifanya ianze kutamba katika ligi hiyo.
Kabla ya mechi za jana, Inter Milan ilikuwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi zake nane ilizovuna katika mechi nne na AC Milan ipo nafasi ya 10 kwenye msimamon wa Serie A ikiwa na pointi tano tu.
Inter Milan inaingia kwenye mechi hiyo kibabe ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Italia dhidi ya watani wao wa jadi, ikifunga mabao nane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.
Zote mbili zimeanza na mwendo wa kinyonga msimu huu ambapo Inter Milan katika mechi zake tano za mashindano tofauti ambazo imecheza hivi karibuni, imeshinda mbili na kutoka sare tatu wakati AC Milan imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare mbili na kupoteza mechi mbili.
Chelsea gari imewaka
Nicolas Jackson na Cole Palmer jana kila mmoja alifunga katika ushindi wa mabao 3-0 wa Chelsea dhidi ya West Ham United ugenini ambao umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 10.
Mwiba kwa West Ham katika mechi ya jana alikuwa ni Jackson ambaye alifunga mabao mawili katika dakika ya nne na 18 na kupika lingine la Cole Palmer katika dakika ya 47 kuihakikishia ushindi timu yake.