Mamlaka ya Kongo yasitisha shughuli za chama cha Joseph Kabila

Mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imesitisha shughuli za chama cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph kabange Kabila cha PPRD. Uamuzi ambao unakuja katika hali ya wasiwasi wakati Bwana Kabila ametoka kutangaza kurejea mashariki mwa DRC.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mamlaka ya Kongo imesitisha shughuli za chama cha rais wa zamani Joseph Kabila, ambacho inakituhumu kwa kudumisha “ukimya wa kina” mbele ya kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kulingana na chanzo cha serikali.

Uamuzi huu unakuja katika hali ya mvutano mkubwa wa kisiasa kati ya serikali ya Kinshasa na kambi ya Bw. Kabila, ambaye hivi karibuni alitangaza kurejea mashariki mwa DRC, eneo linalodhibitiwa kwa sehemu na waasi wa M23.

Shughuli za chama cha PPRD “zimesitishwa katika nchi nzima,” imesema taarifa kwa vyombo vya habari kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani iliyotiwa saini siku ya Jumamosi, Aprili 19.

“Uamuzi huu unafuatia uharakati uliothibitishwa” wa Bw. Kabila, kiongozi wa PPRD, katika “vita hivi vya uchokozi vya Rwanda pamoja na “ukimpya ulikithiri” wa chama chake, andiko hilo linaongeza.

Wizara ya Mambo ya Ndani pia imeshutumu “tabia ya kutatanisha” ya Bw. Kabila, ambaye “hakuwahi kulaani” uasi wa M23, wala uungwaji mkono wa Rwanda kwa kundi hilo linaloipinga serikali.

Pia alilaani “chaguo la makusudi” la mkuu huyo wa zamani la “kurejea nchini kupitia mji wa Goma, ambao uko chini ya udhibiti wa adui, ambaye anamlindia usalama wake.”

Katika taarifa nyingine, Wizara ya Sheria imesema imemwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mahakama ya Juu “kuanzisha kesi za kisheria” dhidi ya Joseph Kabila “kwa ushiriki wake wa moja kwa moja” katika M23.

Chama cha Bw. Kabila hakikujibu mara moja.

Mzozo wa mashariki mwa DRC umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni baada ya kutekwa kwa miji miwili mikubwa katika eneo hilo na kundi la waasi la M23 (“March 23 Movement”), linaloungwa mkono na Rwanda na jeshi lake: Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, na Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini.

Soma piaConstant Mutamba aagiza kesi za kisheria zichukuliwe dhidi ya Joseph Kabila na washirika wake

Rais Félix Tshisekedi, ambaye hadi sasa ameshindwa kupata suluhu la mgogoro huo, mara kwa mara amekuwa akimshutumu mtangulizi wake Joseph Kabila katika miezi ya hivi karibuni kwa kuandaa “uasi” na kuratibu au kuwa mwanachama wa Muungano wa Mto Kongo (AFC), vuguvugu la kisiasa na kijeshi ambalo M23 ni sehemu yake.

Joseph Kabila alitawala DRC kwa miaka 18 (2001-2019) kabla ya kukabidhi madaraka kwa Félix Tshisekedi kupitia makubaliano ya muungano ambayo yalivunjika baada ya miaka miwili.

Wiki iliyopita, timu za idara za kijasusi za kiraia na kijeshi zilifanya msako katika mali ya familia ya Kabila huko Kinshasa, “kutafuta vifaa vya kijeshi au vifaa ambavyo vinaweza kuwa vimeibiwa au kufichwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *