Mamilioni ya Waafrika kuwa masikini kwa sababu ya mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi

Wataalamu wa mabadiliko ya tabia nchi wametahadharisha kuwa mgogoro wa hali ya hewa Afrika utawaelekeza katika umaskini watu wengine zaidi milioni 150 ifikapo mwaka 2050.

Magda Robalo Silva wa Taasisi ya Kimataifa ya Afya na Maendeleo na Waziri wa zamani wa Afya wa Guinea Bissau amesema kuwa mafuriko na ukame vinawalazimisha watu wengi wa Afrika kuyaacha mashamba yao na hivyo kupelekea  watu kukosa lishe bora.

Mafuriko yaliyoikumba Nigeria hivi karibuni

“Hii inasababisha utapiamlo na magonjwa ya kuambukiza katika mataifa mengi ya Afrika. Ikiwa hatutachukua hatua za haraka, watu wengine milioni 150 watasukumwa katika umaskini barani Afrika kabla ya 2050”, ameonya Silva wakati akihutubia kongamano la viongozi huko Dakar mji mkuu wa Senegal kwa minajili ya kuipatia suluhu mgogoro wa mabadiliko ya tabia nchi barani Afrika.

Zaidi ya vijana 100 kutoka mataifa 16 ya Afrika walihudhuria kongamano hilo mjini Dakar, Senegal, lililoandaliwa na Gallen Africa, kikundi cha Afrika nzima kinachohusika na masuala ya afya.

Mataifa mengi ya Afrika, ikiwa ni pamoja na Niger, Chad, Nigeria, Mali, Cameroon, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanakabiliwa na mafuriko makubwa tangu mwezi Juni mwaka huu.