
Mamia ya watu wameshiriki katika maandamano makubwa zaidi dhidi ya Hamas huko Gaza tangu vita na Israel kuanza, wakiingia mitaani kulitaka kundi hilo kuondoka madarakani.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Wanamgambo wa Hamas waliojifunika nyuso zao, baadhi wakiwa na bunduki na wengine wakiwa wamebeba marungu, wameingilia kati na kuwatawanya kwa nguvu waandamanaji hao, na kuwashambulia kadhaa kati yao, kulingana na BBC.
Video zilizosambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii na wanaharakati wanaoikosoa Hamas zimeonyesha vijana wakiandamana katika mitaa ya Beit Lahia, kaskazini mwa Gaza siku ya Jumanne, wakiimba “ondokeni, ondokeni, Hamas”.
Wafuasi wanaounga mkono Hamas wametetea kundi hilo, wakapuuza umuhimu wa maandamano hayo na kuwashutumu washiriki kuwa wasaliti. Hamas bado haijatoa maoni.
Maandamano hayo kaskazini mwa Gaza yamejiri siku moja baada ya watu wenye silaha wa Islamic Jihad kurusha roketi dhidi ya Israeli, na kusababisha Israeli kuchukuwa uamuzi wa kuwataka wakazi kuhama sehemu kubwa za Beit Lahia, jambo ambalo limezua hasira ya wananchi katika eneo hilo.
Israeli imerejelea kampeni yake ya kijeshi huko Gaza kufuatia takriban miezi miwili ya kusitisha mapigano, ikiilaumu Hamas kwa kukataa pendekezo jipya la Marekani la kurefusha muda wa makubaliano hayo. Hamas, kwa upande wake, imeishutumu Israeli kwa kuachana na makubaliano ya awali yaliyokubaliwa mwezi Januari.
Mamia ya Wapalestina wameuawa na maelfu kuyakimbia makazi yao tangu operesheni za kijeshi za Israeli zianze tena kwa mashambulizi ya anga tarehe 18 Machi.
Mmoja wa waandamanaji, mkazi wa Beit Lahia, Mohammed Diab, aliharibiwa nyumba yake katika vita hivyo na kupoteza kaka yake katika shambulio la anga la Israeli mwaka mmoja uliopita.
“Tunakataa kufa kwa ajili ya mtu yeyote, kwa ajenda ya chama chochote au maslahi ya mataifa ya nje,” amesema.
“Hamas lazima ijishushe na kusikiliza sauti ya wenye huzuni, sauti inayotoka chini ya vifusi – ni sauti ya ukweli zaidi.”
Picha kutoka katika jiji hilo pia zinaonyesha waandamanaji wakipiga kelele “Hatuna imani na utawala wa Hamas, hatuna imani na utawala wa Muslim Brotherhood.”
Hamas imekuwa mtawala pekee huko Gaza tangu 2007, baada ya kushinda uchaguzi wa Palestina mwaka mmoja kabla na kisha kuwaondoa wapinzani kwa nguvu.
Ukosoaji wa wazi dhidi ya Hamas umeongezeka huko Gaza tangu vita vilipoanza, mitaani na mtandaoni, ingawa bado kuna wale ambao ni waaminifu sana na ni vigumu kutathmini kwa usahihi jinsi uungwaji mkono kwa kundi hilo umebadilika.
Kulikuwa na upinzani dhidi ya Hamas muda mrefu kabla ya vita, ingawa sehemu kubwa ilibaki imefichwa kwa kuhofia kulipizwa kisasi.
Vita huko Gaza vilichochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo karibu watu 1,200, haswa raia, waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Israel ilijibu shambulio hilo kwa mashambulizi ya kijeshi huko Gaza kuangamiza Hamas, na kuua zaidi ya Wapalestina 50,000, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema.
Wengi wa wakazi milioni 2.1 wa Gaza pia wameyakimbia makazi yao, wengi wao mara kadhaa.
Takriban 70% ya majengo huko Gaza yameharibiwa au kubomolewa kabisa, mifumo ya afya, maji na vyoo hakuna tena, na kuna uhaba wa chakula, mafuta, dawa na makazi.