Mamia ya mashabiki wa Simba wamejitokeza katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kuipokea timu hiyo inayorejea leo Aprili 28, 2025 kutoka Afrika Kusini.
Ikiwa Afrika Kusini, timu hiyo imefuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutoka sare tasa na Stellenbosch ya huko jana Jumapili, matokeo ambayo yameifanya itinge fainali kwa ushindi wa bao 1-0.
Mashabiki hao ambao wamejazana nje ya mlango wa kutokea abiria uwanjani hapa wameonekana kuvalia jezi za timu hiyo hasa za rangi nyekundu, wengine nyeupe na pia za rangi ya bluu.
Nyimbo mbalimbali za kuisifu timu hiyo zimekuwa zikiimbwa na mashabiki hao ambao wamekuwa wakizidi kumiminika kutoka maeneo tofauti Dar es Salaam.
Wapo mashabiki wengine ambao wamekuja na ngoma na gari la muziki lakini wengi wameonekana wakiwa na tarumbeta ndogo maarufu kama vuvuzela.

Kazi kubwa imekuwa ikifanywa na askari wa jeshi la Polisi na walinzi wa usalama uwanjani hapa kuwasimamia mashabiki hao ili kusiwe na usumbufu kwa abiria na watu wengine ambao wamekuja kwq shughuli tofauti uwanjani hapa.
Simba imetinga kwa mara ya pili hatua ya fainali ya mashindano ya klabu Afrika baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la CAF mwaka 1993.