Mameya hao wakiwa na wajumbe wa mabaraza ya miji walimtaka Trump siku ya Jumatano (Juni 11) aache kutumia jeshi pamoja na mawakala wa uhamiaji kwenye msako wake kwa wahamiaji.
Meya wa Los Angeles, Karen Bass, alisema uvamizi huo umezusha fadhaa kubwa ili tu kuiridhisha Ikulu ya White House.
Soma zaidi: Kamatakamata Los Angeles kufuatia amri ya kutotoka nje
“Nakuomba Rais Trump, na tafadhali nisikilize, wacha kabisa kuwatisha wakaazi wetu. Unapaswa kuachana na uvamizi huu.” Alisema Naibu Meya wa Paramount, Brenda Olmos, ambaye mwenyewe alipigwa kwa risasi ya mpira, akizungumza na waandishi wa habari.
Sehemu ya mitaa ya mji huo ilianza utekelezaji wa amri ya kutotoka nje usiku wa Jumanne, lakini eneo linalohusika lina ukubwa wa maili moja tu ya mraba, ilhali mji wenyewe mzima una mailli 500 za mraba.
Operesheni ya kijeshi yaendelea
Kiasi cha wanajeshi 500 waliotumwa kwenye maandamano ya Los Angeles wamepewa mafunzo ya kuwasindikiza maafisa wa uhamiaji kwenye operesheni ya kuwakamata wale Trump anaowaita wahamiaji haramu.
Watu waliokamatwa kwenye msako huo wa nchi nzima, wakiwemo waomba hifadhi, watu waliokaa muda mrefu zaidi ya vibali vyao na wahamiaji hao wanaoitwa haramu wanangojea uamuzi wa mahakama, huku wakishikiliwa kwenye jela zilizosambaa kote nchini Marekani.
Soma zaidi: Polisi yakamata idadi kubwa ya watu Los Angeles
Kwa mujibu wa kamanda wa operesheni hiyo, Meja Jenerali Scott Sherman, japokuwa maandamano yamepunguwa katika maeneo kadhaa ya Los Angeles, lakini hakuwa na hakika ikiwa wanajeshi watasimamisha shughuli waliyoletewa hapo.