Mamelodi, Esperance kitanzini CAF kisa vurugu

Mamelodi Sundowns na Esperance huenda kila moja ikajikuta ikikumbana na adhabu kali kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya mashabiki wa timu hizo kufanyiana vurugu katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini.

Katika mchezo huo, Sundowns iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Peter Shalulile katika dakika ya 54 akimalizia pasi ya Jayden Adams.

Ni mchezo ambao haukumalizika vizuri kutokana na mashabiki wa timu hizo mbili kupigana mara baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa huku chanzo cha vurugu hizo kikiwa hakijulikani.

Mashuhuda wa vurugu hizo wamedai kuwa baadhi ya mashabiki walipata majeraha katika tukio hilo ambayo hata hivyo yalikuwa madogo na madhara hayakuwa makubwa kwa vile Polisi na walinzi wa usalama uwanjani hapo waliwahi kudhibiti.

Katika tukio hilo, mmoja wa mashabiki wa Mamelodi Sundowns anaonekana akitoa msaada wa kumnasua shabiki wa Esperance ambaye alikuwa ananing’nia katika nguzo ya jukwa mojawapo la uwanja wa Loftus Versfeld.

Baadhi ya picha zinaonyesha mashabiki wa Esperance wakiwa wamekusanyika katikati ya Uwanja wa  Loftus huku wakiwa chini ya ulinzi mkali mara baada ya vurugu hizo kudhibitiwa lengo lakiwa ni kuwaepusha zaidi na vurugu kutoka kwa mashabiki wa Sundowns.

Adhabu kali zimekuwa zikitolewa kwa timu mbalimbali kwenye mashindano ya Klabu Afrika zikiwemo kutozwa faini ya hadi Dola 100,000 au timu kuadhibiwa kucheza mechi zake za nyumbani bila mashabiki.

Ikumbukwe Januari mwaka huu, CAF iliipa Simba adhabu ya kucheza mechi moja ya mashindano ya Kombe la Shirikisho pamoja na faini ya fedha kiasi cha Dola 40,000 kwa kosa la mashabiki wake kufanya vurugu kwa mashabiki wa CS Sfaxien katika mechi baina ya timu hizo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Desemba 15, 2023.

Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Kibu Denis.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *