SAFU za ulinzi kwa timu zote sita zinazotarajia kuchuana leo zina vibarua kupunguza makosa kutokana na timu hizo kuchuana kwa safu mbovu kutokana na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nyingi.
Lakini pia washambuliaji wa timu hizo pia watakuwa na kazi ya kufanya kuvuka kuta hizo kutokana na wao pia kutokuwa na ubora wa kufumania nyavu kwa timu zote .
Kwa timu zinazotarajia kucheza, leo Kagera Sugar itakayokuwa wenyeji wa Pamba Jiji safu yake ya ulinzi ndio inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi zaidi kwani katika mechi 22 ilizocheza imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 30 huku ikifunga mabao 16, Pamba wao wamefungwa mabao 23 na kufunga 13 kati ya mechi 22.
Tabora United mzani wao uko sawa, katika mechi 22 walizocheza wamefunga mabao 26 na kufungwa 26 wakati kwa upande wa wageni wao JKT Tanzania na wao mzani wao sawa sawa wamefunga mabao 16 na kufungwa 16.
Dodoma Jiji itakuwa nyumbani ikiikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri inashuka dimbani ikiwa tayari imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 27 huku ikifunga mabao 22 wakati Coastal Union imefungwa mabao 23 na kufunga mabao 18.

Tabora Utd v JKT TZ
Ni mchezo wa mapema saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambapo wenyeji Tabora wanautumia uwanja huo kwa mara ya kwanza baada ya bodi ya ligi kuufungia uwanja wao wa nyumbani waliokuwa wanautumia awali, wanashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa kukubali kipigo cha mabao 4-2.
Lakini pia inashuka dimbani ikiwa imetoka kupata matokeo mazuri katika mchezo wake wa mwisho kabla ya kuvaana na JKT Tanzania leo ambayo imetoka kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya KenGold.
Tabora United inayoshika nafasi ya tano, imeizidi pointi 10 JKT Tanzania iliyopo nafasi ya sita. Hiyo inatoa majibu ya kwamba mchezo huo utakuwa ni wa kujiimarisha tu kwani hautakuwa na timu ambayo endapo itashinda itasogea juu kwani wenyeji wakishinda watafikisha pointi 40 na kuzidiwa pointi moja na Singida Black Stars ambayo ipo nafasi ya nne.

Kagera Sugar V Pamba Jiji
Uwanja wa Kaitaba Kagera Sugar itaikaribisha Pamba Jiji saa 1:00 usiku.Ni mchezo ambao Kagera Sugar inahitaji kupata ushindi ili kujikwamua kwenye nafasi mbovu iliyopo na haitakuwa rahisi kwani inakutana na timu ambayo pia haipo kwenye nafasi nzuri.
Kagera Sugar haina rekodi nzuri nyumbani ikiwa ndio timu iliyokusanya pointi chache (16) sawa na KenGold inayoburuza mkia utofauti ni idadi ya mechi imeshinda mechi tatu, sare saba na vipigo 12 ikikusanya pointi 16 kwenye michezo 22.
Februari 14, 2024 Kagera Sugar ndio mara yao ya mwisho kupata ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani ilipoitandika Fountain Gate mabao 3-0 sasa inakutana na Pamba ambayo imetoka kupoteza nyumbani kwa kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Yanga.
Kwenye mchezo huu timu ambayo itapata matokeo itasogea nafasi moja juu kutoka nafasi iliyopo, Pamba ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 22 ikishinda itaishusha Namungo ambayo ina pointi 23, Kagera iliyo nafasi ya 15 kwa pointi 16 ikishinda itafikisha pointi 19 na kuishusha Tanzania Prisons.

Dodoma Jiji V Coastal Union
Ni vita ya nafasi kwenye mchezo huu unaozikutanisha timu ambazo zimeachana kwa pointi chache hivyo mshindi kati yao atapanda na kumshusha mwenzake. Wenyeji Dodoma Jiji wapo nafasi ya saba kwa pointi 26 wakati Coastal Union ipo nafasi ya tisa kwa pointi 24, ikishinda inafikisha 27 na kuishusha Dodoma Jiji.
Dodoma Jiji inashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutoka kupoteza dhidi ya Tabora United bao 1-0, wakati Coastal Union imetoka kuambulia suluhu na Namungo ugenini.
Mechi tano zilizopita kwa timu zote mbili Dodoma Jiji inaonekana kuwa na ubora zaidi ya Coastal, ikishinda mechi mbili, imefungwa mbili na sare moja wakati Coastal wao wamepoteza mbili na kuambulia sare tatu.
WASIKIE MAKOCHA
Kocha msaidizi wa Tabora United, Halfan Mbonde amesema vijana wake wapo tayari kwa ushindani wataingia kwa kumuheshimu mpinzani wao lakini wanahitaji pointi tatu muhimu ili kuendelea kumuwinda Singida Black Stars katika nafasi ya nne.
“Tupo vizuri na tayari kwa mchezo, tumewafuatilia wapinzani wetu na kutambua ubora na udhaifu wao, dakika 90 zitaamua nani bora zaidi ya mwingine, lakini sisi tumejiandaa kukusanya pointi zote bila kujali mazingira mapya ya uwanja.”
Nahodha wa JKT Tanzania, Edward Songo alisema wamejiandaa kwenda kushindana na kusaka pointi tatu muhimu huku akiweka wazi kuwa hawategemei mshambuliaji kuwapa matokeo.
“Suala la kufunga ni la kila mchezaji hata beki akipata nafasi ya kufanya hivyo anatakiwa kufanya kazi yake kwa usahihi, naamini kocha kafanya kazi yake kilichobaki ni sisi kumaliza kwa kucheza dakika 90 za ubora.”
Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime alisema michezo ya mzunguko huu ni ya kupambania nafasi hivyo wanachofanya ni kumsoma mpinzani ubora na udhaifu wake ili kufanyia kazi kitu ambacho tayari wamekifanya.
“Tunaingia tukiwa na matarajio makubwa ya kupata matokeo mazuri baada ya kumsoma mpinzani na mzunguko huu wa lala-salama sio kupamba kwa ubora ni kupambania pointi tatu muhimu.”
Kocha wa Coastal Union, Juma Mwambusi alisema ligi ni ngumu na ushindani ni mkubwa wanapambana kusaka pointi tatu lakini hata moja sio haba ugenini.