Mambo yanayosubiriwa kwa Amorim United

MANCHESTER, ENGLAND. Jumatatu ya wiki ijayo, kocha mpya wa Manchester United Ruben Amorim  anatarajiwa kuwasili jijini Manchester tayari kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Mashabiki na wadau mbalimbali wa soka duniani wanasubiri kwa hamu kuona nini atafanya msimu huu katika mechi zilizobakia ikiwa pamoja na mabadiliko ya timu kiuchezaji.

Baada ya mchezo wake wa mwisho akiwa kocha wa Sporting Lisbon alipoiongoza timu hiyo ya Ureno kuichakaza Manchester City kwa mabao 4-1 katika Ligi ya Mabingwa, tayari yameonekana baadhi ya mambo ambayo yanaweza kubadilika ama anaweza kuyaingiza katika kikosi cha Man United.

Jambo la kwanza linalo onekana kuwa linaweza kutokea ni idadi kubwa ya mashambulizi ya kushtukiza yatakayokuwa na kasi.

Katika mchezo wao dhidi ya Man City, Amorim na Sporting yake ilikuwa na uwezo wa kuhama kutoka nusu yao hadi lango la mpinzani ndani ya sekunde sita.

Kipindi cha Ole Gunnar Solskjaer, Man United ilikuwa ikifanya sana mashambulizi ya kushtukiza lakini asilimia kubwa yalikuwa hayazai matunda kwa sababu ya kasi.

Mabadiliko kutoka eneo la nusu yao hadi lango la adui hayakuwa yakifanyika kwa kasi kubwa, hivyo inaonekana kuna uwezekano mkubwa Amorim akaibadilisha timu na kuongeza kasi zaidi pale inapokuwa inashambulia.

Jambo zuri kwa Man United ni kwamba ina wachezaji wenye kasi ambao wanacheza eneo la ushambuliaji kama Marcus Rashford na Alejandro Garnacho  ambao kocha huyu anaweza kuwasaidia kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa usahihi zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kitu chapili ambacho kocha huyu anaweza kufanya kusaidia kurudisha ubora wa wachezaji ambao wamekuwa katika viwango vibovu tangu kusajiliwa kwao kwenye timu hiyo.

Hii ni moja kati ya changamoto kubwa ambazo kocha Erik ten Hag alikuwa akikumbana nazo ambapo Mason Mount hajafanya vizuri `hata pale anapokuwa hana majeraha, Antony ambaye amesajiliwa kwa pesa nyingi naye amekuwa na wakati mgumu tangu kuwasili kwake kama ilivyo kwa  Joshua Zirkzee.

Amorim anaonekana kuwa bingwa kufanya wachezaji watoe kile walichonacho, kwani ameshafanya hivyo Sporting akiwa Viktor Gyokeres ambaye alisajiliwa akitokea Coventry City ya Ligi Daraja la kwanza nchini England. Ndani ya msimu wake wa kwanza tu, staa huyu alifunga mabao 43.

Wakati anasajiliwa licha ya kwamba alikuwa amefunga mabao 23 katika msimu wake wa nyuma, hakukuwa na imani kubwa juu yake lakini Amorim alifanikiwa kutengeneza mazingira ya kumfanya awe bora.

Mashetani wekundu kwa sasa wanapata wakati mgumu katika eneo lao la ushambuliaji ingawa ujio wa Amorim unaweza kumaliza tatizo hilo kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kimfumo yakayowawezesha wachezaji kama  Rasmus Hojlund, ambao hawajafikia matarajio ya mashabiki wa timu hiyo tangu asajiliwe.

Kocha huyu pia ni bingwa wa kupindua meza, alifanya hivyo, dhidi ya Man City na  PSV Eindhoven, ndani ya msimu huu ambapo timu yake inapokuwa inaongozwa, huwa inafanya pressing ya hali ya juu na kutoruhusu timu pinzani itengeneze mashambulizi.

Man United chini ya Ten Hag kwa msimu huu imechukua pointi tatu tu katika mechi tisa za ligi ambazo ilianza kwa kuongozwa, pia tangu kuanza kwa  mwaka huu imeshinda mechi mbili tu za Ligi Kuu ambazo yakwanza ni ile ya Sheffield United iliyopigwa April na Brentford, Oktboba.

Chini ya Ten Hag, muda mwingi Man United ilikuwa ikirui hovyo zaidi baada ya kwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza jambo ambalo kwa Amorim ni tofauti na anaweza likaonekana mara atakapoanza kuifundisha timu hiyo.

Kielelezo cha suala hili kwa Ten Hag ilikuwa ni mchezo wake wa mwisho ambapo alichapika na West Ham mabao 2-1.

Katika mchezo wake na Man City Amorim alithibitisha hilo, baada ya kuanza vibaya kipindi cha kwanza na kurudi vizuri zaidi katika kipindi chapili.

“Kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu sana kwetu, na kilichotusaidia ni kwamba tulikuwa na bahati.”