Usiku wa jana ulikuwa na mambo mengi, wakati mechi ya watani wa jadi wa Jiji la Liverpool, Everton na Liverpool ilikuwa ya mwisho kabisa kupigwa kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Mechi hii ya Ligi Kuu England ilikuwa na mambo mengi furaha, huzuni, shangwe, vurugu na historia ya aina yake wakati Everton ikilazimisha sare ya mabao 2-2 na wapinzani wao hao wa jadi.
Bao la kusawazisha la dakika ya 89 la James Tarkowski, liliihakikishia Everton alama moja, lakini pia limekuwa na maana kubwa kwao huku ikiinyima Liverpool fursa ya kuandika historia ya aina yake kwenye uwanja huo na kwenye ‘Merseyside Derby’.

Kama Everton ingepoteza ingekuwa ni maumivu zaidi kwao kwani mechi ya jana ilikuwa ya mwisho ya watani wa jadi wa Merseyside kuchezwa katika Uwanja wa Goodison Park kwa vile baada ya msimu huu kumalizika, utabomolewa na kujengwa mpya ambao Everton itautumia kwa mechi zake za nyumbani.
Kabla ya timu hizo kukutana jana, zilikuwa zimecheza mechi 82 za watani wa jadi wa Merseyside ambapo kila moja imepata ushindi mara 41, hivyo ambayo ingepata ushindi jana maana yake ingeondoka na historia tatu ya ubabe katika mechi baina yao uwanjani hapo.
Ni mechi iliyoshuhudiwa refa Michael Oliver akitoa kadi nne nyekundu, mbili kwa wachezaji Curtis Jones wa Liverpool na Abdoulaye Doucoure wa Everton huku wengine wawili wakiwa ni kocha wa Liverpool, Arne Slot na msaidizi wake Sipke Hulshoff.
Sare hiyo imeifanya Liverpool iendelee kuongoza msimamo wa EPL ikifikisha pointi 57, saba zaidi ya zile za Arsenal inayoshika nafasi ya pili wakati Everton imepanda hadi katika nafasi ya 15 ikifikisha pointi 27.

Lakini Goodison Park ni uwanja wa namna gani, una historia gani ya ajabu chini ni namba kuhusu dimba hilo lenye rekodi kubwa barani Ulaya.
133- Miaka ambayo Uwanja wa Goodison Park umetumika tangu ulipojengwa mwaka 1892.
39,414– Idadi ya mashabiki wanaoingia kwenye Uwanja wa Goodison Park.
3,000- Kiasi cha pauni kilichotumika kwa ajili ya matengenezo ya uwanja huo kipindi hichO.
11- Mabao mengi ambayo yaliwahi kufungwa kwenye mchezo mmoja katika uwanja huo wakati Everton iliposhinda 9-2 dhidi ya Sheffield Wednesday.
78,299– Idadi ya mashabiki wengi kuwahi kuingia kwenye uwanja huo kwa wakati mmoja, mechi ilikuwa kati ya Everton na Liverpool, mwaka 1948.
05- Mechi tano za Kombe la Dunia zilipigwa kwenye uwanja huu mwaka 1966.
15- Mechi ambazo Everton iliwahi kushinda nyumbani mfululizo, kuanzia Oktoba 4,1930 hadi Aprili 4, 1931.

47– Idadi ya mechi ambazo Everton walifunga mabao mfululizo kuanzia Aprili 23, 1984 hadi Septemba 2, 1986.
6-Jack Southworth wa Everton anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mechi moja katikati uwanja huo baada ya kufunga sita wakati timu yake ilipovaana na West Bromwich Albion Desemba 30, 1893.
3, 703– Hawa ni mashabiki wachache zaidi kuwahi kuingia kwenye Uwanja wa Goodison Park wakati timu hiyo ikivaana na Millwall mwaka 1988.
01– Mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Bolton Wanderes na Notts County ilipigwa hapa mwaka 1894.
04- Mechi nne za mchezo maarufu wa Rugby zimewahi kupigwa kwenye uwanja huu tangu ulipofunguliwa rasmi.