Mambo sita yaisubiri Kamati Kuu Chadema

Kakola. Mambo sita likiwemo la makada na viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia (Chadema) kujivua uanachama mfululizo zinatarajia kutawala katika kikao cha kamati kuu ya chama hicho Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho, ambacho kitakuwa cha kwanza kufanyika bila kuwepo Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye yupo mahabusu, kitaongozwa na Makamu Mwenyekiti, Bara, John Heche.

Hoja zingine zinazotarajiwa kuchukua muda mwingi ni barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa juu ya kutowatambua wajumbe wa kamati kuu na sekretarieti, akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika pamoja na makovu wa uchaguzi wa ndani wa chama hichoo uliofanyika Januari 21, 2025.

Masuala mengine ni kesi ya Lissu na ile ya madai inayohusiana na mgawanyo wa raslimali za chama pamoja na kushukilizwa kwa muda Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa akiwa safarini kwenda Ubelgiji kuhudhulia mkutano wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU).

Aidha, ajenda ya jumla ya ni hali ya kisiasa ikijikita kwenda operesheni wanayoiendesha ya No reforms no election, bila shaka kikao hicho hakiwezi kumalizika bila kuigusia.

Uwepo wa kikao cha kamati hiyo, ulitangazwa na Heche usiku wa jana Ijumaa, Mei 16, 2025 alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha ndani na wanachama wa Chadema Family, katika Kijiji cha Kakola wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Bila kutaja ajenda, Heche alisema kikao hicho kitajadili mambo kadhaa ya ustawi na mikakati ya chama, ikiwemo mwendelezo wa kampeni ya ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ inayoendelea katika kanda mbalimbali.

“Kuna watu eti wanadai Chadema inakufa…Chadema hii hii tunayoitisha mkutano wa hadhara saa 2:00 asubuhi na watu wanajitokeza hadi mtu anakosa pa kukanyaga ndio inakufa? Wanajidanganya sana,” amesema Heche.

Kujivua uanachama

Kikao hicho kitafanyika katika kipindi ambacho misukosuko inayoikumba Chadema, suala kujivua uanachama huenda likatawala kutoka historia ya tangu kuanzishwa kwa chama hicho, haijawahi kutoka makada na viongozi waandamizi kuhama chama hicho kwa maelezo yanayofanana.

Kundi la kwanza la kutangaza kujivua uanachama lilikuwa la waliokuwa wajumbe wa sekretarieti likiwahisha John Mrema, Salum Mwalimu, Benson Kigaila, Catherine Ruge na Julius Mwita waliodai kuchoshwa na uongozi wa Lissu ulivyoshindwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Baada ya kina Mrema na wenzake kuondoka, ndipo mfululizo wa mikutano kati ya  wanahabari, makada na viongozi wa Chadema wakiwemo wajumbe wa kamati kuu, baraza kuu, mkutano mkuu, wenyeviti na makamu wenyeviti wa kanda, mikoa na wilaya, pamoja na viongozi wa mabaraza.

Kwa ujumla wao wote waliondoka hawajaweka bayana wapi wanaelekea, badala yake wanasema wanatafuta jukwaa mbadala la kuendeleza harakati ingawa taarifa zinadai uelekeo wao ni Chaumma kinachoongozwa na Hashim Rungwe, na kuwa walitarajiwa kutambulishwa leo kwenye vikao vya juu ambavyo hata hivyo, inadaiwa vimeahirishwa.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka kwa wandani wa Chaumma ni kwamba Jumatatu ya Mei 19, 2025 jijini Dar es Salaam kutofanyika kamati kuu na halmashauri kuu ambavyo vitatumika kuwapokea waliojindoa Chadema.

Hamahama hiyo ikiendelea, kamati kuu ya Chadema itakuwa na kibarua cha kujadili kwa kina hali hiyo, kisha kutoa maelekezo na mikakati ya kuikabili na kupanga tarehe za uchaguzi ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

Tayari Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameelekeza nafasi za viongozi waliohama zijazwe haraka ili kuimarisha muundo wa chama hicho, kuboresha shughuli zake na kuendeleza harakati.

Barua ya Msajili

Mbali na hilo, barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyokitaka Chadema kuitisha upya baraza kuu kuthibitisha upya wajumbe wanane wa kamati kuu na sekretarieti, ingawa Chadema inasema suala hilo haliko ndani ya mamlaka ya msajili, lazima lijadiliwe na kupatiwa suluhisho la ndani.

Agizo la Msajili lililenga kujibu malalamiko yaliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome, akipinga akidi ya Baraza kuu iliyowathibitisha viongozi hao walioteuliwa na mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Mchome alikuwa akilalamikia kwamba akidi haikutimia ya kuwathibitisha viongozi hao, akisema ilihitaji asilimia 75 ya wajumbe halali, huku chama hicho kikisema akidi hiyo hutumika tu katika uchaguzi na kupitisha masuala ya kisera, na kuwa suala hilo lilihitaji asilimia 50 ya wajumbe ambao walitimia

Viongozi waliolalamikiwa Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Wengine ni wajumbe wa kamati kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, kupitia mikutano yake Heche amesisitiza mara kadhaa kuwa hakuna watakachokibadilisha kwa kuwa bado wanawatambua Mnyika na wenzake kama viongozi halali.

Golugwa kukamatwa

Moja ya mambo makubwa yaliyojitokeza karibuni ni hatua ya Polisi kumkamata Golugwa Mei 13, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akiwa safarini kwenda Brussels nchini Ubelgiji kushiriki mkutano wa IDU, uliofanyika Mei 14, ambako pamoja na mambo mengine suala la Lissu kukamatwa na kushatakiwa lilikuwa moja ya ajenda.

Hata hivyo, salamu za Golugwa katika mkutano zilifikishwa na mke wa Lissu, Alicia Magabe huku Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, likitaja sababu za kumshikilia Golugwa kuwa “ni mwenendo wake wa kusafiri kwa siri kwenda nje na kurudi nje ya Tanzania.”

Makovu ya uchaguzi

Kwa kuwa sekeseke la makada wa chama kuondoa linakolezwa na makovu ya uchaguzi na yapo madai kuwa uongozi umeshindwa kuwaunganisha wanachama, inatazamiwa kamati kuu kujadili hali hiyo na kuitafutia dawa kabla haijaendelea kukipasua chama. Katika uchaguzi huo Lissu alishinda kwa kura 513 sawa na asilimia 51.5 huku Mbowe aliyekuwa akitetea akipata kura 482 sawa na asilimia 48.3.

Baada ya uchaguzi huo ulionekana mgawanyiko wa wazi wa pande mbili, moja ikiwaunga mkono walioshinda na mwingine Mbowe, ambao umekuwa ukilalamika kutengwa na kubaguliwa.

Katika hatua nyingine huenda Katibu Mkuu wa Baraza Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo akatoa mrejesho kwenye kikao hicho kuhusu mchakato wa kurudisha hali ya umoja na mshikamano kupitia mazungumzo walioyafanya kwa Mbowe na Lissu katika kutafuta muafaka na maridhiano.

Kesi ya Lissu

Ingawa kesi Lissu linaendelea na Jumatatu zitaitwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, suala hilo lazima litajadiliwa kwa kina katika kikao hicho, kuweka mikakati ya kisheria na mingine kuhakikisha mwenyekiti huyo anarejea uraiani.

Pia kuna wanachama waliojeruhiwa na polisi baada ya kukamatwa mahakamani, nao watakuwa sehemu ya mjadala kuhusu namna ya kuwasaidia.

Vilevile, kama alivyodokeza Heche, watajadili hali ya mwenendo wa operesheni ya No reforms no election ambayo kwa mara kwanza ilizinduliwa Kanda ya Nyasa ya Chadema (Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa na Songwe), ikaelekea Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Mtwara) kisha kanda ya Pwani mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kisha ikaenda Victoria (Mwanza, Geita na Kagera), Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *