
Kuna mtu aliwahi kunukuliwa akisema, ‘watoto ni watu wazima wenye miili midogo.’ Hakuwa amekosea.
Huu ni ukweli ambao wengi wetu tunachelewa kuufanyia kazi. Ingawa hawawezi kusema wazi wazi, watoto wana mahitaji wasiyoweza kuyasema wazi, lakini tusipoyachukulia kwa uzito yanaweza kuleta madhara makubwa na kuharibu kabisa mwelekeo wa maisha yao.
Unaweza, kwa mfano, kumwambia mtoto neno la kumkejeli na huenda humaanishi lakini jambo hilo likawa sumu mbaya isiyosahaulika.
Unaweza kumwambia, ‘huna akili’, ‘mjinga wewe’ kama namna ya kusema hajafikiri vizuri lakini hujawaza namna neno hilo linavyoingia kwenye ufahamu wake.
Tunatambua kuwa jukumu letu wazazi ni kuwasaidia watoto kujenga mtazamo sahihi wa maisha utakaowasaidia kuwa na mtazamo chanya na maisha, kujiamini na hata kuwa na nguvu ya kufanya mambo makubwa katika maisha.
Kwa msingi huo katika makala haya, nimechagua mambo sita ninayoamini mtoto akiyasikia kwa mzazi wake anajenga mtazamo chanya na maisha yake.
‘Ninakupenda’
Unaweza kumpa mtoto vitu vingi, lakini kamwe huwezi kumpa mtoto upendo tofauti na kumdekeza mtoto. Unampenda mtoto kwa kumuonesha kwa maneno na vitendo kuwa ana umuhimu kwako kama mzazi wake.
Najua hili si jepesi kwa wazazi wengi. Pamoja na vitendo, tunawajibika kusema kwa maneno kuwa tunawapenda.
Mtoto akishaamini unampenda atakuwa na ujasiri na furaha. Bila kuwa na uhakika kuwa unampenda, mtoto hukosa utulivu wa nafsi na wengine wanaweza kutumia nafasi hiyo vibaya.
‘Wewe ni wa thamani’
Hakuna binadamu anayevumilia kupuuzwa. Mtu wa kwanza kumthibitishia mtoto kuwa yeye ni wa thamani ni mzazi wake. Hili, kwa hakika, linajenga mtazamo chanya na nafsi yake. Moyo wake unashiba na tabia zake zinatulia.
Unapojitahidi kupatikana kwa mtoto, kuzungumza naye na kumsikiliza, kimsingi unakuwa umemwambia yeye ni wa thamani. Unaweza kumuonya mtoto bila kumfanya ajione hana thamani. Unaweza kuadhibu tabia yake bila kumfanya ajione hana maana. Ujumbe wa ‘mimi ni wa thamani’ unapaswa kuanzia kwa mzazi.
‘Nisamehe nimekosea’
Mtoto anahitaji kusikia ukikiri makosa yako. Hupotezi mamlaka yako kwa kumwambia mtoto kweli umekosea. Unapokubali kuwa umekosea, unapanda mbegu njema ya kuomba msamaha.
Ukimwambia mwanao nisamehe, unamwonesha kuwa na wewe ni binadamu unayeweza kukosea na atakuamini zaidi.
Sambamba na kumwomba msamaha, unahitaji kujenga tabia ya kumsamehe. Mtoto anapokukosea, onesha mfano wa kuachilia. Kosa lisiwe sababu ya kuvunja uhusiano wako na mwanao.
‘Ninakusikiliza’
Tabia nyingi za ovyo tunazoziona kwa watoto wetu, mara nyingi ni kilio cha kutafuta kusikilizwa au kukata tamaa kuwa hakuna anayesikiliza.
Pamoja na udogo wao, watoto wanapenda sana kujua kuwa wanasikilizwa. Kumsikiliza mtoto kunagusa moyo wake. Kusikilizwa kunamfanya ajisikie unajali na kumheshimu kama binadamu timamu.
Kumsikiliza mtoto ni pamoja na kuvumilia mawazo yake. Ingawa ni vizuri kutoa maelekezo ya nini afanye muda wote, unaweza pia kumpa nafasi ya kusema mawazo yake hata kama unadhani hayana mantiki. Kusikiliza maana yake ni kumpa usikivu.
‘Unawajibika’
Unakutana na watu wanaopenda kubebesha wengine lawama, saa nyingine, hata kwa makosa yao wenyewe. Wapo pia wale wavivu wenye tabia ya kuwalalamikia na kuwakosoa wale wanaojaribu kufanya kitu. Watu hawa hawajajifunza kuwajibika.
Mtu mwajibikaji, kwa kawaida, anajua kile anachotakiwa kukifanya. Unapokuwa mwajibikaji hutegemei watu wengine wafanye badala yako; hutafuti mtu wa kumlaumu mambo yanapokwenda mrama; huogopi kufanya uamuzi na kuwajibikia uamuzi huo.
Mfundishe mtoto uwajibikaji kwa kujenga tabia ya kuongozwa na malengo anapofanya majukumu uliyompa. Pale anaposhindwa kufikia malengo, au hata pale anapokosea, mwajibishe na aone matokeo ya kutokufikia malengo aliyonayo.
Pia, mpe mtoto fursa ya kufanya uamuzi unaomhusu. Usimfanye awe mtu anayesubiri kuambiwa nini cha kufanya kila wakati. Pale anapohitaji mawazo, msaidie bila kummnyang’anya uhuru wake.
‘Bidii ni msingi wa mafanikio’
Tunao watu wazima wanaoamini mafanikio huja kwa muujiza. Wanafikiri kufanikiwa ni bahati na ‘kismati’ hivyo ili ufanikiwe lazima uombewe au basi upate msaada wa ‘nguvu za giza.’ Mawazo kama haya yamefanya watu wengi watumie muda mwingi kudanganyika kuliko kufanya kazi.
Ukweli ni kwamba bila bidii na kujituma hakuna mafanikio. Hakuna mafanikio yanayopatikana kwa njia za mkato. Tunahitaji kuingiza mawazo haya kwa watoto wetu.