Mambo matatu ubabe wa Simba, Yanga KMC Complex

Msimu uliopita, Simba na Yanga zilitumia Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam kwa mechi zao za nyumbani za Ligi Kuu baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa.

Hata hivyo msimu huu, timu hizo mbili kwa nyakati tofauti ziliamua kuukimbia Uwanja wa Azam Complex na kutimkia Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam kwa ajili ya kuutumia kwa mechi zao za nyumbani.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kusogea KMC Complex ambapo ilifanya hivyo kabla ya ligi kuanza na baadaye Yanga ikafuata mara baada ya kucheza mechi tano za nyumbani katika Uwanja wa Azam Complex.

Uamuzi wa Simba na Yanga kukimbilia KMC Complex hadi sasa umeonekana kuwa na faida kwa timu hizo hasa kwenye Ligi Kuu.

Hatoki mtu

Tangu Yanga na Simba zilipoanza kucheza mechi zao za mashindano ya ndani katika Uwanja wa KMC Complex, hakuna hata moja iliyowahi kuonja ładha ya kupoteza mechi uwanjani hapo tofauti na wenyeji KMC ambao tayari wameshapigika mara tatu katika mechi 10 walizocheza hapo.

Yanga imecheza mechi sita katika uwanja huo ambapo tano ni za Ligi Kuu na imeshinda zote huku moja ikiwa ya Kombe la Shirikisho la TFF nayo imeshinda.

Simba imecheza mechi tisa ambapo nane ni za Ligi Kuu ambazo imeshinda saba na kutoka sare moja na moja ni ya Kombe la Shirikisho la TFF ambayo imeshinda.

KMC wenye Uwanja wao, wamecheza mechi 10 za ligi, wakishinda tano, sare mbili na wamepoteza tatu na wamecheza mechi moja ya Kombe la Shirikisho la CRDB na wamepata ushindi.

Mabao yamiminika

Katika hali ya kushangaza, Yanga na Simba zote zimefunga idadi sawa ya mabao katika mechi za Ligi Kuu ambazo zimecheza kwenye Uwanja wa KMC Complex, kila moja ikiwa nayo 22.

Yanga imefunga mabao 22 katika mechi tano ikiwa ni wastani wa mabao 4.4 kwa mchezo na Simba imefunga mabao 22 katika mechi nane ikiwa ni wastani wa mabao 2.8 kwa mechi.

Katika Kombe la Shirikisho la CRDB, Yanga imecheza mechi moja na kufunga mabao matano huku Simba ikifunga mabao sita.

Wenyeji KMC wao katika mechi 10 za ligi walizocheza kwenye Uwanja wao wa KMC Complex, wamefunga mabao nane ikiwa ni wastani wa bao 0.8 kwa mechi.

KMC katika Kombe la Shirikisho la CRDB wamecheza mechi moja na wamefunga mabao matano.

Ukuta wa Chuma

Yanga katika mechi sita ilizocheza kwenye Uwanja wa KMC Complex, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu ikiwa ni wastani wa bao 0.5 kwa mechi.

Simba katika mechi tisa ilizocheza katika Uwanja wa KMC Complex, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili ikiwa ni wastani wa bao 0.2 kwa mechi.

KMC ukuta wake unaonekana kuvuja sana katika Uwanja wa KMC Complex kwani katika mechi 11 za mashindano ilizocheza hapo imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13 ikiwa ni wastani wa bao 1.2 kwa mchezo.