Mambo manne yaliyoteka mjadala bajeti ya elimu

Mambo manne yaliyoteka mjadala bajeti ya elimu

Dodoma. Mambo manne yameteka mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2025/26, ikiwemo fedha za miradi ya maendeleo kutotolewa kwa wakati.

Nyingine ni mdondoko wa wanafunzi, miundombinu ya shule, upungufu na utaratibu unaotumika katika kuajiri walimu.

Hata hivyo, mbali na dosari hizo,  Bunge lilipitisha Sh2.4 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele vitano kwenye bajeti hiyo,  huku Serikali ikiongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Bajeti hiyo iliyopitishwa Mei 12,2025, ni ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti ya mwaka 2024/25 ambayo ilikuwa ni Sh1.97 trilioni. 

Kwa upande wa fedha za kugharamia miradi ya maendeleo, fungu limeongezeka kwa asilimia 32 kutoka Sh1.32 trilioni katika mwaka 2024/25 hadi Sh1.74 trilioni mwaka 2025/26.

Ilichosema Kamati ya Bunge

Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, inasema kutopatikana kwa fedha zlizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kunaathiri malengo na madhumuni ya miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa mwaka huo.

“Hali ya jumla ya upokeaji wa fedha za kugharamia miradi imekuwa nzuri kutokana na mchango wa fedha za nje kuliko fedha za ndani,”anasema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Husna Saiboko.

Hata hivyo,  anasema upokeaji wa fedha za ndani hauonyeshi mwenendo mzuri hadi kufikia Februari, 2025 fedha zilizopokelewa ni asilimia 55 tu.

Kamati hiyo inataka fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitolewe kwa ukamilifu kabla ya Juni 30 mwaka 2025.

Ingawa kuna changamoto ya upatikaji wa fedha kwa wakati katika miradi na ongezeko la bajeti,  bado wadau wa elimu likiwamo Shirika la HakiElimu wanataka ongezeko la bajeti ya elimu lifikie asilimia 15 ya bajeti kuu ya Serikali ili kupunguza changamoto mbalimbali.

Ajira, upungufu wa walimu

Mbunge wa Urambo, (CCM) Margaret Sitta anashauri Serikali kuangalia upya utaratibu wa kuwapata walimu wapya katika ajira zake, kwa kuwa wamesoma na kisha kufanya mitihani na kuhoji sababu ya kuwapa tena usaili na mitihani.

“Watu wanaohitimu chuo halafu wakapitishwa tena katika mitihani, naomba hili tuliangalie upya. Hivi  kweli kuna umuhimu wa kuwapitisha walimu tena kwenye mitihani wakati walishakaa vyuoni?”anahoji.

Suala hilo la kutofanya mitihani kwa walimu ambalo liliungwa mkono na wabunge wengi, lilizungumzwa pia na Mbunge wa Singida Mjini (CCM) Mussa Sima  aliyesema kuna uhaba wa walimu 268,000.

Sima anasema hivi karibuni Serikali iliajiri walimu 14,000 lakini kwa mtindo wa kufanya mitihani kabla ya ajira jambo hilo linasikitisha kwa kiasi kikubwa.

“Mwalimu anapaswa kupimwa darasani, hapaswi kupimwa katika mitihani, eneo hili kwa kweli hata mimi sikuwa nimelipenda,”anasema.

Maoni ya Sima ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo yanashabihiana na vuguvugu la Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Nchini (NETO) ambao wanalalamikia kuwapo Kwa mitihani wakati wa usaili wa kada hiyo.

Kwa upande wake,  Mbunge wa Muleba Kusini (CCM) Charles Mwijage anashauri Serikali kufanya uamuzi mgumu wa kuwaajiri walimu wote 268,000 wanaohitajika katika shule mbalimbali nchini.

“Tujifungie tujiulize, tukiajiri walimu 268,000 nini kitatokea? Tuna walimu 268,000 wanatakiwa na sia ajabu tunao mtaani, tukiamua kama Taifa kwamba tunakwenda kuwaajiri tutakosa nini tukae katika vipaumbele vyetu, vingine tuache,”anasema.

Mwijage anasema kuna nchi moja iliwahi kukopa Benki ya Dunia kwa ajili ya kulipa walimu lakini hivi leo wanafanya vyema katika maendeleo.

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi za Jamii na Elimu (FAHE) katika Chuo Kikuu cha St John, Dk Shadidu Ndossa anasema kutumia walimu wa kujitolea kungeweza kupunguza changamoto, lakini hilo bado halijafanyika, ingawa kuna walimu wengi wako mitaani wangeweza kufanya hilo.

“Jambo jingine ni utekelezaji wa policy (sera) yetu mpya ambayo inataka walimu waende internship (mafunzo kwa vitendo), kama wataitekeleza  tutaona matunda yake mwaka 2028 au 2029,”anasema.

Anasema kama Sera  itasimamiwa vyema, kila mwaka kutakuwa na walimu kama 20,000 ama 30,000 ambao wataenda mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja na kufanya mgawanyo mzuri itakapofika wakati huo.

Dk Ndossa anashauri pia matumizi ya Tehama yatakayowezesha walimu kufundisha shule zaidi ya moja.

Miundombinu na mdondoko wa wanafunzi 

Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza anashauri Serikali kufanya utafiti kuhusu suala la mdondoko kwa kuwa kuna takwimu tofauti zinazotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Baraza la Mitihani Tanzania  (Necta)

“Fanyeni utafiti kujua ukubwa wa tatizo hilo, kama nilivyosema Rais Samia Suluhu Hassan amejenga shule nyingi lakini hatujui hawa watoto wanapotelea wapi, mfanye utafiti na uje na jibu,” alimwambia waziri.

Mbunge wa Hanang,  Samwel Hayuma anashauri kujengwa kwa mabweni ili kukabiliana na mdondoko wa wanafunzi unaotokana sababu kadhaa ikiwamo umbali mrefu kwenda na kurudi shule.

“Watoto wa kike wanapata ujauzito kwa sababu ya mazingira magumu, wengine wamepangisha kwenye geto, tumejenga shule sasa tuangalie jinsi tunavyoweza kuboresha  mazingira yetu,”anasema.

Anasema badala ya kujenga shule nyingi katika kata moja, Serikali iangalie jinsi ya kuboresha miundombinu ili wanafunzi waweze kusoma.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje anasema bado hadi leo Tanzania imekuwa ikijadili upungufu wa matundu ya choo na kwamba angetamani ifike muda suala hilo liishe tena kwa shule kuwa vyoo vya kisasa.

“Tena viwe  vyoo vya kisasa, kwa sababu tuna teknolojia na mifumo, tuna mipango na vipaumbele kwanini tusilimalize hili liiishe tuwe tumebaki na maintenance ( ukarabati) wa vyoo tu,”anasema Nusrat.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kuteuliwa (CCM) Vuai Ali Nahodha anasema upo msongamano mkubwa wa wanafunzi na kuwa, kwa uzoefu wake hakuna mwalimu anayeweza kufundisha darasa lenye watu zaidi ya 50. 

“Ili kukabiliana na msongamano wanafunzi wagawanywe katika makundi mawili, kundi la kwanza la wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza la pili na tatu waingie darasani kwa utaratibu wa kawaida kuanzia saa 1.00 asubuhi na wale darasa la nne hadi la sita wawekwe katika ukumbi mkubwa wa mikutano,”anasema.

Mbunge wa Singida Mjini (CCM) Mussa Sima, anasema katika bajeti hiyo hajaona maandalizi ya miundombinu kwa kuzingatia matokeo ya wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza mwaka 2028, ambapo watakutana wanafunzi wanaoishia darasa la sita.

Wadau wengine

Mwalimu wa Shule ya Msingi jijini Dodoma,  Zainab Yamlinga anasema mambo ambayo yanachangia mdondoko ni malezi, migogoro baina ya wazazi, maradhi ya muda mrefu kwa watoto na kukosekana kwa vifaa kwa watoto wenye mahitaji maalumu.

Anasema walimu nao wanatakiwa kufundisha kwa moyo, kuwafariji wanafunzi na kuwa wabunifu kwa sababu kufanya vibaya darasani kunaweza kuwa ni chanzo cha utoro.

Zainab anasema mwanafunzi anapofeli na kusemwa kwa lugha mbaya anachukia walimu, kusoma na hata shule yenyewe.

Mipango ya Serikali 

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia wizara hiyo imepanga kutekeleza vipaumbele vitano kwa kutumia bajeti iliyopitishwa.

Anataja vipaumbele hivyo ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo.

Vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu.

Anataja  vipaumbele vingine kuwa ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu, kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Anasema juhudi zaidi zitatumika kupeleka vijana wa Kitanzania kusomea mambo ya sayansi ya nyuklia, mambo ya kompyuta na akili-unde kwenye vyuo bora vilivyo nje ya nchi.

Kuhusu elimu ya juu, alisema Serikali itaendelea kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wenye sifa ili kuongeza fursa za elimu ya juu nchini.

Anasema Serikali itaongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu kutoka 245,314 mwaka 2024/25 hadi wanafunzi 252,773 kwa mwaka 2025/26.

Anasema kati ya hao mwaka wa kwanza ni  88,320 na wanaoendelea ni 164,453 .

Pia anasema Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 wa ngazi ya stashahada katika fani 86 za kipaumbele kama sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *