
Bravos do Maquis inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola imejikuta katika wakati mgumu kwenye Ligi hiyo baada ya kuendelea kupata matokeo yasiyoridhisha, huku ikiwa inajiandaa na mchezo wa kwanza wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba.
Bravos mpaka sasa imecheza mechi 10 za Ligi Kuu ya Angola ambapo imeshinda mechi tatu, imepata sare tano na imepoteza mechi mbili huku ikishika nafasi ya sita ikiwa imekusanya pointi 14.
Mechi ya kwanza ilipoteza ikiwa nyumbani kwa mabao 2-0 dhidi ya Bingwa mtetezi wa Lgi hiyo Atlético Petróleos de Luanda wakati mchezo wa pili ilipoteza ugenini dhidi ya G.D. Interclube kwa mabao 3-1. Katika michezo 10 ya Ligi iliyocheza, Bravos imefunga mabao 11 huku ikiruhusu mabao 10.
Bravos ilifanikiwa kuingia katika hatua ya makundi baada ya kucheza mechi nne dhidi ya timu mbili katika hatua za awali huku mchezo wa kwanza ilikutana na Coastal Union ambapo ilifanikiwa kupata ushindi wa jumla wa mabao 3-0.
Mechi ya kwanza ilichezwa Angola ambapo Bravos ilishinda mabao 3-0 wakati mechi ya pili ilipata sare ya 0-0 ilipokuwa ugenini kwenye uwanja wa Azam Complex dhidi ya Coastal Union.
Baada ya kuiondoa Coastal Union kwenye hatua za mtoano, Bravos ilikutana na Saint-Éloi Lupopo ya DR Congo ambapo mechi ya kwanza Bravos ikiwa ugenini ilipata ushindi wa mabao 2-1 huku mechi ya marudiano iliyochezwa Angola, Bravos ilishinda tena bao 1-0 ikipata ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na kufanikiwa kufuzu hatua ya makundi.
Bravos imepangwa kundi A dhidi ya Simba, Constantine ya Algeria, pamoja na CS Sfaxien ya Tunisia ambapo mechi ya kwanza hatua ya makundi itakutana na Simba Novemba 27, 2024 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.