Dar es Salaam. Ukiachana na uwezo wake kimuziki, wengi wanamuheshimu Alikiba kutokana na kuweza kuendelea kuwepo katika muziki tena akifanya vizuri kwa kipindi kirefu ukilinganisha na wasanii wengi aliotoka nao kipindi kimoja.
Ametoa albamu na EP, ameshinda tuzo za ndani na kimataifa, nyimbo zake zinapata namba kubwa mtandaoni huku akianzisha rekodi lebo yake ya Kings Music ambayo imeshafanya kazi na wasanii sita hadi sasa. Fahamu zaidi.
Alikiba alikaa miaka 10 bila kumshirikisha msanii yeyote wa kike katika wimbo wake, tangu alipotoa kolabo yake na Lady Jaydee, Single Boy (2012), hakufanya hivyo hadi alipokuja kumshirikisha Sabaha Salum katika wimbo wake, Yalaiti (2023).

Hata hivyo, kwa kipindi hicho Alikiba alikuwa akishirikishwa na wasanii wa kike kutoka ndani na nje, miongoni mwao ni Nandy (Nibakishie), Maua Sama (Niteke Remix), Maud Elka (Songi Songi Remix) n.k.
Alikiba alichukua usikivu wa wengi katika Bongofleva baada ya kuachia albamu yake, Cinderella (2007) chini ya G Records, kisha zikafuata Ali K4Real (2009) na Only One King (2021) pamoja na EP moja, Starter (2024).
Tayari Alikiba ameshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) mara 18 akiwa msanii wa pili aliyeshinda tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 chini ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata).
Rapa kutokea Classic Music Group (CMG), Darassa katika albamu mbili alizotoa, Slave Becomes a King (2020) na Take Away The Pain (2025), Alikiba ndiye msanii pekee Bongo aliyeshirikishwa katika albamu zote mbili.
Hadi sasa wimbo wa Alikiba, Mahaba (2023) ulioshinda tuzo ya TMA, video yake ndio iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda mfupi sana ikizipita video za nyimbo zake nyingine kama Mwana (2014), Seduce Me (2017) na Utu (2022).
Ni Alikiba ambaye video ya wimbo wake, Seduce Me (2017) ilitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 1 ndani saa 37 ikiivunja rekodi ya wimbo wake Diamond Platnumz, Salome (2016) uliofikisha milioni 1 kwa saa 48.
Alikiba ameshinda tuzo za kimataifa kama All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible), pia alishinda MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2016 kama Msanii Bora Afrika.
Katika albamu yake, Only One King (2021) yenye nyimbo 16, Alikiba alifanya video za nyimbo nane ambazo ni Infidele, Ndombolo, Salute, Jealous, Oya Oya, Bwana Mdogo, Utu na Niteke, hivyo kuandika rekodi kama albamu iliyotoa video nyingi kwa mwaka huo.
Only One King ilizizidi albamu zilizotoka mwaka huo kama Sound From Africa (Rayvanny), Defination of Love (Mbosso), High School (Harmonize), Air Weusi (Weusi), 20 (Lady Jaydee), Asante Mama (Dogo Janja), Experience (Stereo), The Gift of Life (Best Naso) n.k.
Wimbo wa Dully Sykes, Zali (2024) unaofanya vizuri kwa sasa, wote umeandikwa na Alikiba ambaye kashirikishwa, Dully alimpa Kiba nafasi hiyo maana anajua soko la muziki kwa sasa linataka kitu gani.
Na Dully Sykes anaamini kuwa Alikiba ndiye mfalme wa Bongofleva kwa sababu ni msanii wa kwanza ambaye alikuwa bado hajatoka kimuziki lakini akamuomba amshirikishe katika wimbo wakati tayari yeye alikuwa msanii mkubwa wakati huo.
Ni Dully anayejitaja kama mwanzilishi wa Bongofleva akiwa ametoa albamu tatu hadi sasa, Historia ya Kweli (2002), Handsome (2004) na Hunifahamu (2005).

Tangu ametoka kimuziki zaidi ya miaka 10 iliyopita Maua Sama hajatoa albamu ila ameachia EP mbili, Cinema (2022) na Sama (2024), na katika EP zote Alikiba ameshirikishwa na ndio msanii pekee Bongo aliyepata nafasi hiyo kwa Maua.
Ikumbukwe Maua Sama alitoka kimuziki baada ya kuachia wimbo wake, So Crazy (2013) akiwa na Mwana FA ambaye naye aliwahi kumshirikisha Alikiba katika wimbo wake, Kiboko Yangu (2014) ulioshinda tuzo ya TMA kama Wimbo Bora wa Kushirikiana 2015.