Dar es Salaam. Mama wa aliyekuwa mwigizaji Hawa Hussein ‘Carina’ amesema uvimbe tumboni ndiyo ugonjwa uliomuua mwanaye.
Mama huyo ameiambia Mwananchi leo Jumatano Aprili 16, 2025 kuwa ugonjwa huo umemsumba Hawa kwa miaka nane.

“Mwanangu alikuwa na uvimbe tumboni basi ndio chanzo, akakatwa tumbo hadi kafariki kafanyiwa upasuaji mara 26. Na tatizo likawa linajirudia ndiyo maana zikawa operesheni nyingi.
“Nimebaki na kumbukumbu ya kwamba jana nimeongea naye vizuri sana lakini kumbe sikujua kama anakufa. Ameugua karibia miaka nane ameacha mtoto mmoja anaitwa Aisha,” amesema mama wa marehemu.
Hata hivyo ametoa shukrani kwa Watanzania waliomshika mkono tangu mwanaye alipoanza kuugua.

Utakumbuka Hawa alionekana kama Video Queen kwenye wimbo wa ‘Oyoyo’ wa kwake Bob Junior lakini pia alicheza kwenye tamthilia ya kwanza ya mwigizaji Jacob Stephen ‘JB’ ya mwaka 2017 hadi 2018 iliyoitwa ‘Kiu ya Kisasi’.

Carina alifariki dunia jana Aprili 15, 2025 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu. Hata hivyo mwili wake utawasili nchini Ijumaa Aprili 18,2025, kisha utapumzishwa Jumamosi Aprili 19, 2025 katika makaburi ya Kisutu.