
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Desemba 2, 2024 kuwasomea hoja za awali (PH) Sophia Mwenda (64) na mwanaye, Alphonce Magombola (36) wanaokabiliwa na kesi ya mauaji.
Mwenda ambaye ni mkazi wa Mbagala anadaiwa kushirikiana na mtoto wake huyo wa kiume, kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kumzaa mwenyewe.
Uamuzi huo umetolewa leo, Novemba 18, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga.
Hakimu Kiswaga amepanga tarehe hiyo, baada ya wakili wa Serikali, Roida Mwakamele kuoimba Mahakama hiyo ipange tarehe kwa ajili ya Serikali kuwasomea washtakiwa maelezo yao.
Kiswaga alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, 2024.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi ya mauaji kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Julai 15, 2022 na kusomewa kesi ya mauaji namba 3 ya mwaka 2022.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la mauaji Desemba Mosi, 2020, eneo la Kijichi wilaya ya Temeke.
Inadaiwa siku hiyo usiku, Mwenda na Alphonce wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni mwana familia na kinyume cha sheria.
Washtakiwa baada ya kusomewa shitaka linalowakabili siku hiyo, hawakurusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.