Maluma: Winga wa Ndanda aliyeibukia kwenye ngumi

FELIX Theodory Maluma ni mmoja kati ya mabondia chipukizi wa mchezo wa ngumi za kulipwa anayepambania ndoto yake kupitia mchezo huo baada ya kuachana na mchezo soka.

Maluma ambaye kiasili ni mwenyeji wa mkoa wa Mtwara akitokea katika kijiji cha Ndanda  lakini mabadiliko na utemi wa jiji la Dar es Salaam ukamfanya ageukie mchezo wa ngumi za kulipwa nchini.

Bondia huyo anayecheza katika uzani wa walter akiwa ameshapanda ulingoni katika mapambano saba ambayo sawa na raundi 26 akiwa ameshinda matatu kati ya hayo mawili kwa Knockout.

Bondia huyo amepigwa mara mbili kati ya hizo moja ikiwa ni kwa Knockout huku akiwa ametoka sare mara mbili.Maluma kwa sasa anakamata nafasi ya 17 katika mabondia 58 wa uzani wa Walter  nchini wakati duniani akiwa wa 788 katika mabondia 2460 huku akiwa na hadhi ya nyota moja.

Maluma amefanya mahojiano maalum na Mwananchi ambapo ameeleeza safari yake ya maisha katika mchezo huo ilivyoanzia akitokea katika mchezo wa soka.

“Safari yangu imeanzia katika mchezo wa soka kijijini kwetu Ndanda ambacho kipo mkoani Mtwara, nimecheza namba ya 11 ambayo ni winga wa kushoto.

“Nimecheza katika timu ya Ndanda na kabla ya hapo nimeshiriki mashindano ya umitanshuta kutoka ngazi ya mkoa hadi ya kitaifa.

“Unajua sikuwa kabisa na mpango wala kuwahi kuwaza kucheza ngumi kwa sababu ndoto yangu ilikuwa kwenye mpira lakini kuna wakati fulani nilikosa mchujo wa kwenda nje kwa sababu nilipata kazi ya kupeleka abiria Masasi.

“Mbali ya kucheza soka katika timu ya Ndanda nilikuwa pia naendesha bodoboda sasa baada ya kukosa nafasi kwenda nje niliamua kuja kutafuta maisha katika jiji la Dar es Salaam,” alisema bondia huyo.

Kazi yangu kubwa Dar es Salaam ilikuwa kuuza  viatu vya mitumba katika soko la Manzese, nakumbuka wakati huo barabara ilikuwa ile moja, hakuna Mwendokasi, maisha yangu yalikuwa hivyo.

“Sasa wakati nipo Dar nikawa pia nachukuliwa kwenda kucheza mechi ndondo ambazo nilikuwa nalipwa shilingi 10,000 au 15000  ndiyo nikakutana na kocha Mbago akaniambia niachane na mpira niende kucheza ngumi.

“Kilichosababisha aniambie hivyo ni kutokana na mwili wangu aliona unafaa kuwa bondia lakini nilimueleza sitoweza napenda sana mpira ila yeye akaniambia nikiwa tayari niende.

“Wakati nafanya biashara Manzese, kulikuwa na mambo ya utemi, alikuwa Thoma Mashali na Idd Bonge lakini  Mashali alikuwa anafanya kazi ya kuchangisha shilingi 1000 katika kila meza.

“Watu waliowatuma walivyofika kwenye meza yangu niligoma kutoa hiyo pesa, wakanifanyia fujo kwa kuvunja meza na kutupa barabarani viatu nilivyokuwa na nauza wakati huo Manzese barabara moja.

“Lakini wakaona haitoshi wakaenda kumwambia Mashali ambaye alikuja akanipiga sana na sikuweza kumrudishia kwa sababu sikuwa na uwezo wa kupigana.

“Binafsi baada ya tukio lile ndiyo nilienda kwa kocha Mbango kujifunza ngumi ili kuweza kujilinda kwa matukio ambayo nilikuwa nakutana nayo.

“Nilifanya mazoezi kwa yule kocha katika kipindi kifupi kwa sababu alikuwa na asili ya uganga wa dudu wake walimkataza nikamwambia anitafue mwalimu wa ngumi karibu na eneo langu la biashara ndiyo akaniambia niende kwa kocha Edward Lyakwipa’ kocha Eddo’ wa Sifa Boxing Club anapotokea Idd Pialali,” alisema

Umelipwa pesa nyingi mara ngapi kwenye ngumi?

“Kiukweli sijawahi kulipwa pesa yoyote zaidi ya kukwambia mpaka sasa nimecheza mapambano yangu bure kwa sababu naijenga rekodi yangu.

“Huenda pengine kwa sasa ndiyo naweza nikalipwa laki mbili au tatu kwa sababu nina nyota moja lakini bado sijaanza kupata faida kwenye huu mchezo.

Nini kwa upande wako kimekuwa changa moto kwenye ngumi?

Kikubwa ni namna ya kuweza kujigawa na kusababisha mambo yakaenda kwa sababu familia unakuta inahitaji huduma na mchezo pia unakuhitaji jambo ambalo linakufanya wakati mwingine upande mmoja kukosa msaada wa kutosha.

“Lakini kwa upande wangu bado nina ndoto ya kuweza kufika mbali katika mchezo huu, nimekuwa nikipambana kuhakikisha hilo jambo linafanikiwa katika hali yoyote, nashukuru makocha wangu wa Sifa Boxing Club wamekuwa sehemu ya maisha kwa kutupa miongozo mizuri.

“Naamini kuwa huko mbele nitafanya vizuri zaidi kwa kuwa nimekuwa na juhudi sana za kufanya mazoezi na mwalimu wangu amekuwa akinisimamia vizuri, hivyo baada ya muda utaniona kwenye majukwaa makubwa ya ngumi duniani.”