
Moshi. Aliyekuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Godfrey Malisa, amewasilisha maombi kortini akiomba uanachama wake ulindwe, ili afungue maombi ya kupinga mchakato wa kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais.
Dk Malisa amewasilisha ombi hilo akiomba mahakama itoe zuio la muda kwa lengo la kulinda hadhi ya uanachama wake, wakati maombi yake ya kupinga uteuzi huo wa Rais yakiwa bado hayajafunguliwa.
Ombi hilo limewasilishwa likiambatanishwa na kiapo cha wakili Emanuel Anthony, akiomba yasikilizwe kwa dharura, kwa kuwa mteja wake anakusudia kuishtaki Bodi ya Wadhamini ya CCM na watu wengine kuhusiana na uamuzi huo.
Kulingana na hati ya wito ambayo Mwananchi inayo, imewataka wajibu maombi katika shauri hilo, kufika mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Proches Mushi, Aprili 24, 2025 saa 3:00 asubuhi wakati maombi yatakaposikilizwa chemba.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, alipotafutwa kwa simu leo Jumanne, Aprili 8, 2025, na kuulizwa kama ana taarifa juu ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, alijibu kwa kifupi:
“Jamani, mimi naomba msinishirikishe kwenye mambo ya huyo mtu.”
Katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika jijini Dodoma, Januari 18 na 19, 2025, wajumbe wa mkutano huo walimpitisha Rais Samia kuwa mgombea urais na Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mbali na uteuzi huo ambao awali haukuwamo kwenye agenda, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM pia walipitisha jina la Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kuwa mgombea urais wa Zanzibar 2025.
Hata hivyo, baada ya shughuli hiyo, Dk Malisa, aliyejiunga na CCM mwaka 2020, alijitokeza hadharani akipinga uteuzi huo akidai ulikiuka Katiba ya CCM. Februari 10, 2025, CCM ikamfuta uanachama kada huyo.
“Malisa amefukuzwa kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CCM kwa sababu amekuwa akibeza uamuzi uliofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Januari 19, 2025,” alinukuliwa Mercy Mollel akitangaza uamuzi huo.
Maombi ya Malisa yanasemaje
Katika maombi hayo, Dk Malisa ameishtaki Bodi ya Wadhamini ya CCM kama mjibu maombi wa kwanza, na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambayo ilitangaza kumfuta uanachama, kama mjibu maombi wa pili.
Dk Malisa katika maombi hayo, amedai anaweza kuthibitisha kuwa Katiba ya CCM na utaratibu wa kumpata mgombea, Rais Samia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025 ulikiukwa na chama hicho.
Kada huyo amesema yeye ni mwanachama wa CCM tangu Novemba 2020, na ana kadi ya uanachama namba C00004714-016-1, iliyotolewa Novemba 20, 2020.
Kwamba Januari 19, 2025, CCM kilifanya mkutano na katika mkutano huo, Rais Samia aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais, na kwa kuwa suala hilo halikuwa kwenye agenda, kada huyo hakuridhishwa na uamuzi huo.
“Kutoridhishwa kwangu ni kwa sababu kulikiuka taratibu. Kutokana na kukiukwa huko kwa taratibu, nilikiomba chama changu (CCM) kupitia vyombo vya habari kufuta uamuzi huo na kurudi kufuata taratibu.
“Pia niliwajulisha viongozi wa chama changu juu ya nia yangu ya kwenda mahakamani ili uteuzi huo utenguliwe,” ameeleza na kuongeza kuwa wakati akisubiri majibu, alishtushwa na taarifa kwamba amefukuzwa uanachama.
“Binafsi sijawahi kupewa huo uamuzi. Hakukuwa na mwenendo wowote wa mashitaka dhidi yangu…,” ameeleza na kuongeza kuwa kwa mshangao aliona kupitia YouTube tangazo la kufutwa kwake uanachama.
“Kwa hiyo, ninakusudia kufungua maombi kupinga utaratibu uliotumiwa na CCM baada ya kufuata taratibu zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na kumpelekea notisi Rais.
“Hii itawezekana tu kama uanachama wangu utalindwa, kwani bila hivyo sitaweza kudai haki yangu ya kisiasa na kiraia kupinga ukiukwaji huo wa taratibu. Kumshtaki Rais katika kesi ya madai kunahitaji nimtumie Rais notisi,” ameeleza Malisa katika maombi hayo.
Dk Malisa ameeleza kuwa Februari 11, 2025, aliandika barua kwenda kwa Rais akimjulisha nia yake ya kukifungulia kesi ya madai chama chake, na barua hiyo .aliituma Machi 13, 2025 akiwa ameambatanisha nakala yake.
“Nina ushahidi kuthibitisha kuwa Katiba ya CCM ilikiukwa,” ameeleza katika maombi hayo na kuambatanisha Katiba ya CCM ya mwaka 2022, na kueleza kuwa katika shauri atakalofungua, ataomba zuio la kufutwa uanachama.
Dk Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010, alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia TLP. Mwaka 2015, aligombea urais kupitia CCK na baadaye kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2018, aligombea ubunge Kinondoni kwa chama cha TLP, na mwaka 2020 aligombea ubunge wa Moshi Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi, lakini kote huko kura zake hazikutosha.