Mali zilizotokana na dawa za kulevya kutaifishwa

Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, imetoa tamko la kutaifisha mali za watuhumiwa wanne wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh976.05 milioni ambazo zimethibitika kuchumwa kiharamu kupitia dawa hizo.

Kamishna wa mamlaka hiyo, Kanali Burhani Zuberi Nassoro amesema anataifisha mali hizo kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 73 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, sheria namba nane ya mwaka 2021 na baada ya kuzingatiwa matakwa ya kifungu cha 71 cha sheria hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 11, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Unguja.

Kanali Nassoro amewataja watuhumiwa ni Saleh Khamis Baslema, mkazi wa Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi na mkewe, Gawar Bachi Fakir ambao wanataifishiwa mali zenye thamani ya Sh422.126 milioni.

Mali zitakazotaifishwa ni viwanja, magari na pikipiki.

Aprili 22, 2024 watuhumiwa hawa walitaifishiwa pia mali zao nyingine zenye thamani ya Sh15.3 bilioni kutokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Mtuhumiwa mwingine anayetaifishiwa mali zake ni Mohamed Abdulla Juma,  mkazi wa Michenzani Unguja aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kada ya sheria.

Mali inayotaifishwa ni kiwanja chenye thamani ya Sh35 milioni.

Kanali Nassoro amesema mtuhumiwa amebainika kutumika kufanya utakatishaji wa fedha za mtuhumiwa mkubwa wa dawa za kulevya Basleman na mkewe Gawar. 

“Pia imebainika ndiye aliyeingiza nchini simu za satellite zilizotumika kuwasiliana na manahodha wa meli kutoka Afhanistani waliyoingiza dawa za kulevya Zanzibar na Tanzania kwa jumla,” amesema Kanali Nassoro. 

Mtuhumiwa mwingine ni Andreas Wolfgang Fretz, raia wa Ujerumani ambaye ametaifishiwa mali zake zenye thamani ya Sh518.926 milioni ambazo gari na nyumba mbili.

Kanali Nassoro amesema mtuhumiwa alikamatwa Oktoba 17, 2023 saa 4:00 asubuhi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa mtuhumiwa ameanzisha kilimo cha kisasa cha dawa za kulevya aina ya bangi mseto (skanka) Kijiji cha Paje Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja. 

Katika operesheni hiyo, mtuhumiwa alikutwa na mashine ya kisasa ya kuoteshea miche ya bangi, shamba za bangi na bangi iliyovunwa tayari kwa kuifikisha sokoni. 

Kanali Nassoro  amesema tamko hilo linafanyika baada ya kujiridhisha kwamba zipo sababu za msingi za kuamini mali hizo zimepatikana isivyo halali.

“Wahusika walipewa wito wa kuripoti Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kipindi kisichozidi siku 30 kwa ajili ya kuonesha vyanzo vya mapato au mali namna au njia zilizotumika kuzipata mali hizo,” amesema Kanali Nassoro.

“Pia, kuonesha sababu kwa nini mali hizo zisitamkwe kwamba zimepatikana isivyo halali na kutaifishwa kuwa mali ya Serikali, hata hivyo licha ya tangazo hilo watuhumiwa hawakuripoti.”

Kanali  Nassoro amesema Serikali imedhamiria kudhibiti dawa za kulevya Zanzibar kwa mujibu wa sheria bila kuangalia jina, wadhifa au utaifa wa mtu. 

Hata hivyo, amesema iwapo kuna mtu yeyote hajaridhika na tamko hilo anaweza kuiomba Mahakama kufanya mapitio na ombi lake linatakiwa kuwasilishwa kwa kipindi cha siku 30 kunzia sasa.

Mussa Mohamed, mkazi wa Unguja akizungumza na Mwananchi amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali za kukabiliana na biashara hiyo haramu, lakini bado kuna haja ya ushirikishwaji kwa ajili ya kuitokomeza.

“Jitihada zinaonekana lakini bado wanatakiwa kuongea nguvu zaidi kudhibiti hawa watu, wao wanatajirika lakini vijana wanaangamia hapa kisiwani kwa sababu ya kutumia dawa hizo,” amesema Mohamed.