Bunge la Mpito la Mali limepitisha sheria inayojinaisha vitendo vya ufuska vya ‘ushoga’ na kujiunga na makumi ya nchi zingine za Kiafrika zilizopitisha sheria ya kupiga marufuku vitendo hivyo vinavyotetewa na Ulimwengu wa Magharibi kwa kisingizio cha haki za binadamu.
Muswada wa sheria hiyo uliopitishwa na baraza hilo sasa unasubiri kutiwa saini na uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo ili kuwa sheria rasmi.
Akizungumzia kupitishwa muswada huo, Waziri wa Sheria na Haki za Binadamu wa Mali Mamadou Kassogue amesema, “kuna vifungu katika sheria zetu vinavyokataza ushoga nchini Mali”, na akaongezea kwa kusema “yeyote anayejihusisha na tabia hii, au kuishamirisha au kuiunga mkono, atachukuliwa hatua. Hatutakubali mila na maadili yetu yakiukwe na watu kutoka mahali pengine. Maandishi haya yatatumika, Mungu akipenda,” amesisitiza Kassogue .

Msimamo huo wa serikali ya Mali umetangazwa wakati nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinatoa mashinikizo kwa nchi mbalimbali za Kiafrika ya kuzitaka zihalalishe kisheria vitendo vya ushoga kwa kisingizio cha uhuru wa binafsi na haki za binadamu.
Marekani na nchi kadhaa za Ulaya zimesitisha na hata kukata misaada kwa nchi kadhaa za Afrika zilizojinaisha maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, siku ya Alkhamisi Baraza la Taifa la Mpito linalohudumu kama bunge la Mali tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi mwaka 2020, lilipitisha rasimu ya kanuni ya adhabu ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku ushoga kwa kura 132 zilizounga mkono dhidi ya kura moja iliyopinga.
Hadi sasa, nchi zisizopungua 30 za Afrika zimepiga marufuku ‘ushoga’, huku Mauritania, Somalia na Sudan zikiwa zimeweka adhabu ya hukumu ya kifo kwa watu wanaothibitika kufanya vitendo hivyo vya kingono…/